Jul 04, 2020 09:28 UTC
  • Utawala wa Kizayuni; mhusika wa utekaji nyara wa wanadiplomasia wanne wa Iran huko Lebanon

Yapata miaka 38 imepita sasa tangu kutokea tukio la kutekwa nyara wanadiplomasia wanne wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Lebanon.

Sayyid Muhsin Mousavi Naibu Balozi, Ahmad Mutevaselian Mwambata wa Kijeshi katika ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Taqi Rastegar Moghadam Mshauri wa Masuala ya Ufundi wa ubalozi wa Iran huko Beirut pamoja na Kadhem Akhavan ripota wa shirika la habari la IRNA walitekwa nyara na vibaraka wa utawala wa Kizayuni tarehe 5 Julai mwaka 1982 wakiwa katika kituo cha upekuzi  kaskazini mwa Lebanon.   

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana Ijumaa ilitoa taarifa kwa mnasaba wa tukio hilo na kueleza kuwa: "Kama ilivyotangazwa katika miaka yote hii ni kwamba ushahidi na taarifa za kuaminikia zinaeleza kuwa wanadiplomasia hao waliotekwa nyara huko Lebanon walikabidhiwa kwa wanajeshi ghasibu wa utawala wa Kizayuni na kisha wakapelekwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu; na sasa wanashikiliwa katika jela haramu za utawala huo."

Taarifa na ushahidi wa kuaminika kuhusiana na tukio hilo la kigaidi zinaonyesha kuwa wanamgambo waliokuwa wakiongozwa na Elie Hobeika na kisha Samir Geagea kutoka katika kambi za Wazayuni huko Lebanon walihusika katika utekaji nyara huo. Aidha baada ya kutekwa nyara wanadiplomasia hao wa Kiirani walipelekwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na watu hao hao na kukabidhiwa mikononi mwa idara husika za Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad).  

Samir Geagea, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa wanamgambo wa Kifalanja wa Lebanon 

Elie Hobeika alisema kuwa Israel ilitaka wanamgambo wa Kikristo wa Lebanon wawapeleke Israel wanadiplomasia hao wa Kiirani waliotekwa nyara. Naye Samir Geagea ambaye mwaka 1982 alikuwa mmoja wa viongozi wakuu, mwenye kuchukua maamuzi na aliye na ushawishi wa wanamgambo wa Kifalanja na ambaye alikuwa akichukua hatua kwa pamoja na Hobeika katika kalibu ya kundi moja, alithibitisha katika mahojiano aliyofanya Agosti 31 mwaka 1997 na jarida la Al Wasat linalochapishwa huko Lebanon juu ya kushikiliwa watu hao na maajenti wa utawala wa Kizayuni.  

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon anasema kuhusu jambo hilo kuwa: Zipo ishara kwamba wanadiplomasia hao wa Iran wanashikiliwa katika jela za utawala wa Kizayuni." Israel inadai katika ripoti zake kuwa wanadiplomasia hao wanne wa Kiirani walitekwa nyara na Mafalanja na kwamba waliuawa na wanamgambo hao na miili yao kuzikwa. Israel ni adui yetu, na sisi hatuwezi kuamini ripoti zake hizo. Kama Israel ilivyokuwa ikikadhibisha huko nyuma pia kuhusu kuwepo katika jela zake baadhi ya mateka, lakini imebainika wazi kuwa mateka hao walikuwepo katika jela za utawala huo."  

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon 

Kuna nukta kadhaa katika kadhia hii ya kigaidi.  

Ya kwanza ni kuwa mbeba dhima wa taathira za kitendo hicho cha kigaidi kwa kuzingatia rekodi ulionayo utawala wa Kizayuni katika uwanja anajulikana wazi kabisa na wala hawezi kujificha.  

Nukta ya pili, ni kushikwa na kigugumizi na kukaa kimya Umoja wa Mtaifa na taasisi za kimataifa katika uwanja huo. Kama tukio kama hili lingejiri katika nchi yoyote ya Ulaya au huko Marekani kelele zingesikika na hatua zote zingechukuliwa kuanzia kutumwa jumbe za uchunguzi hadi kutolewa azimio ili kuweka wazi kadhia hiyo.  

Nukta ya tatu ni kuwa tangu awali utawala wa Kizayuni umekuwa ukitumia vitendo vya kigaidi kama wenzo wa kuendeleza uvamizi na chokochoko zake. Ni wazi kuwa Israel ni sababu na chanzo cha  ukosefu wa amani, ushari na vitendo vya ugaidi katika eneo.  

Edward Snowden mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA anasema: utawala wa Kizayuni, Marekani na Uingereza zimeandaa mpango wa pamoja kwa jina la "Pango la Nyuki" na kupitia mpango huo Syria imegeuzwa kuwa kitovu cha kukusanya mamluki wa ugaidi waliotapakaa kote duniani.   

Edward Snowden, mfanyakazi wa zamani wa CIA  

Kwa kuzingatia ushahidi na nyaraka za kuaminika; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajukumika kisiasa na kisheria kufuatilia utekaji nyara huo, na inaamini kuwa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake ndio wahusika wakuu wa kitendo hicho cha kigaidi. Iran inautaka pia Umoja wa Mataifa utekeleze majukumu yake ipasavyo bila ya kuingiza siasa katika suala hilo. 

Maoni