Jul 04, 2020 11:47 UTC
  • Njama mpya za Wazayuni zazidi kuwafanya kitu kimoja Wapalestina

Makundi mbalimbali ya Palestina yamepongeza makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya harakati za HAMAS na Fat'h na kusema kuwa, hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na njama mpya za Wazayuni kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Nafiz Azzam, mjumbe wa Tawi la Kisiasa la Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema leo Jumamosi kwamba, juhudi kubwa sasa hivi zimejikita kwenye kuanzisha mazungumzo ya kitaifa na makubwa baina ya makundi yote ya Palestina na tayari Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeshawasiliana na harakati ya Fat'h.

Amesema, mpango wa kitaifa wa kuunda kambi moja ya ndani itakayoyashirikisha makundi yote ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na changamozo na mashinikizo, lazima ifufuliwe upya na inabidi kambi hiyo iwe na malengo ya muda mrefu baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na makundi mengine ya taifa hilo kwa ajili ya kupambana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Matamshi kama hayo yametolewa pia na Mahir al Tahir, mmoja wa viongozi wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Palestina na Ahmad Hilles, mjumbe wa Kamati ya Wananchi ya Harakati ya Fat'h.

Kambi ya muqawama ndicho kigezo bora cha kupambana na Uzayuni wa kimataifa

 

Wakati huo huo Mahmoud al Zahar, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameiambia televisheni ya al Mayadeen kwamba, taifa zima la Palestina, wakubwa kwa wadogo, vizee kwa vijana, watu wa mirengo na itikadi tofauti, wote wanapaswa kuwa sehemu ya mpango wa ukombozi wa ardhi za Palestina na kuufurusha utawala pandikizi wa Israel. 

Vile vile amekitaka Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO kuweka pembeni makubaliano ya Oslo na kusisitiza kuwa, sasa hivi eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linahitajia kufuata kigezo kile kile cha muqawama kinachofuatwa katika Ukanda wa Ghaza.

Itakumbukwa kuwa, utawala wa Kizayuni ulikuwa na nia wa kuteka ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, jinai ambayo imezidi kuwashikamanisha na kuwafanya kitu kimoja Wapalestina tofauti na walivyotarajia Wazayuni.

Tags

Maoni