Jul 05, 2020 03:46 UTC
  • Spika wa Bunge la Kuwait ataka nchi za Kiarabu zikabiliane na Israel

Spika wa Bunge la Kuwait ametaka nchi za Kiarabu zichukue hatua kali za kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuteka maeneo zaidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Marzouq al-Ghanim, Spika wa Bunge Kuwait amesema utawala wa Kizayuni unapaswa kuchukuliwa hatua kali na nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa kutokana na kitendo cha kukwepa kutekeleza maazimio ya kimataifa hasa, kuhusu ardhi zinazokaliwa kwa mabavu tokea mwaka 1967. Al-Ghanim ameongeza kuwa wabunge wa Kuwait wanapinga kwa nguvu zao zote mpango wa kuteka ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi na njama zote za kiuadui za utawala wa Kizayuni. Aidha wamesema wabunge wa Kuwait wako tayari kushirikiana na mabunge ya nchi za Kiarabu na nchi zingine rafiki pamoja na jumuiya za mabunge ya Asia na kimataifa kwa ajili ya kusitisha njama za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. 

Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umepanga kuanza kutekeleza siku ya Jumatano ya tarehe Mosi Julai mpango wake haramu wa kupora na kuunganisha asilimia 30 ya ardhi za Ufukwe wa Magharibi na ardhi zingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu, lakini ukalazimika kuakhirisha na kusogeza mbele tarehe ya utekelezaji wa mpango huo baada ya kushadidi mashinikizo ya upinzani ya Wapalestina na ya nchi mbali mbali duniani.

Tags