Jul 06, 2020 02:29 UTC
  • Maelfu ya Wairaqi waandamana, walaani gazeti la Saudia kwa kumvunjia heshima Ayatullah Sistani

Maelfu ya Wairaqi wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad wakilaani hatua ya gazeti linalomilikiwa na Saud Arabia la al Sharq al Awsat ya kumvunjia heshima kiongozi mkuu wa kidini nchini humo, Ayatullah Ali Sistani.

Waandamanaji hao walikusanyika katika malango ya eneo la Green Zone linalojumuisha balozi kadhaa za nchi za kigeni na ofisi muhimu za Serikali na Bunge la Iraq wakitaka kuvamia ubalozi wa Saudi Arabia.

Waandamanaji hao pia wameitaka serikali ya Iraq kuchukua msimamo wa wazi dhidi ya hatua hiyo ya gazeti la Saud Arabia ya kumvunjia heshima mwanazuoni na kiongozi huyo wa juu wa kidini.

Vyombo vya usalama vya Iraq vilikuwa na kibarua kigumu cha kudhibiti maandamano hayo na vililazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwazuia waandamanaji kuvamia ubalozi wa Saudia mjini Baghdad.

Wakati huo harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali hatua ya gazeti la al Sharq al Awsat la Saudi Arabia ya kumvunjia heshima Ayatullah Ali Sistani na kusisitiza kuwa, mwanazuoni huyo ana nafasi muhimu katika nyoyo za Waislamu.

Maelfu ya Wairaqi wameandamana mjini Baghdad 

Taarifa ya Hizbullah ya Lebanon imeashiria fatwa iliyotolewa na Ayatullah Ali Sistani akiwataka Wairaqi wa matabaka, dini na madhehebu zote kulinda nchi yao muda mfupi baada ya kudi la kigaidi lililokuwa likisaidiwa na Saudi Arabia, Marekani, Israel na washirika wao, kuvamia ardhi ya Iraq mwezi Juni mwaka 2014.

Taarifa ya Hizbullah imesema hatua ya gazeti hilo linalomilikiwa na Saudi Arabia imechukuliwa kwa ajili ya kudhamini maslahi na malengo ya maadui wa Umma wa Kiislamu wanaoongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Siku ya Ijumaa iliyopita gazeti hilo la utawala wa Aal Saud lilichapisha picha ya katuni iliyomtusi na kumvunjia heshima Ayatullah Sistani, kiongozi wa juu wa kidini mwenye hadhi ya juu nchini Iraq, hatua ambayo imekabiliwa na upinzani na malalamiko ya mirengo na makundi mbalimbali ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo ya kulaani hatua hiyo ya kiafiriti.

Tags

Maoni