Jul 06, 2020 06:10 UTC
  • Marekani yasisitiza, itaendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya Afghanistan

Balozi mdogo wa Marekani mjini Kabul amesema kuwa majeshi ya nchi yake yataendelea kuwepo katika ardhi ya Afganistan.

Ross Wilson amesema wanajeshi wa Marekani hawana nia ya kuondoka Afghanistan na suala hilo halo halimo katika hati ya makubaliano ya amani ya Doha kati ya Washington na kundi la Taliban; hivyo wanajeshi hao wataendelea kuwepo nchini Afghanistan. 

Wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Afghanistan  

Katika makubaliano hayo yaliyotiwa saini miezi minne iliyopita mjini Doha huko Qatar, Washington iliahidi kuwa majeshi yote ya kigeni yaliyoko Afghanistan chini ya uongozi wa Marekani yataondoka katika ardhi ya Afghanistan miezi 14 baada ya kusainiwa makubaliano hayo.

Matamshi yaliyotolewa na balozi mdogo wa Marekani mjini Kabul kuhusu kuendelea kuwepo majeshi ya nchi hiyo katika ardhi ya Afghanistan ni katika fremu ya stratijia inayotekelezwa na ikulu ya rais wa Marekani, White House. Washington inaendeleza stratijia hiyo licha ya kwamba kundi la Taliban linasisitiza kuwa, litaendeleza mapambano yake nchini humo hadi pale wanajeshi wote vamizi wa nchi za kigeni watakapoondoka kikamilifu katika ardhi ya Afghanistan. Hata baada ya kutia saini makubaliano ya Doha tarehe 29 Februari mwaka huu, kundi hilo la Taliban halina imani na ahadi za Marekani kutokana na tabia ya nchi hiyo ya kukiuka makubaliano ya pande mbili na ya kimataifa. Hasa katika kipindi cha sasa ambapo serikali ya Donald Trump imesitisha mipango yake ya kimataifa ikiwemo kadhia ya Afghanistan na suala la kuondoka wanajeshi wake nchini humo kutokana na kuzongwa na migogoro mingi ya ndani kama maafa ya virusi vya corona na maandamano yanayoendelea nchini humo kupinga dhulma na ubaguzi wa rangi.

Ujumbe wa kundi la Taliban 

Msimamo wa Marekani wa kuendelea kuwepo wanajeshi vamizi wa nchi hiyo huko Afghanistan unaweza kukwamisha au kuvuruga kabisa jitihada zinazofanywa na viongozi wa Kabul za kuitisha mazungumzo ya amani na kundi la Taliban na kupelekea kufungwa kikamilifu njia iliyofunguliwa kwa ajili ya mazungumzo ya kisiasa baina ya makundi yote ya Afghanistan. 

Marekani inadai kuwa inataka kubakisha sehemu ya wanajeshi wake nchini Afghanistan kwa ajili ya kuzuia uwezekano wowote wa kundi la Daesh kupata nguvu zaidi nchini humo.

Siku kadhaa zilizopita gazeti la Times lilifichua kwa mara ya kwanza kwamba, hati ya makubaliano ya amani baina ya Marekani na Taliban ina kipengele cha siri kinacholiruhusu jeshi la nchi hiyo kubakisha kikosi cha eti kukabiliana na ugaidi  nchini Aghanistan. Kundi la Taliban halijatoa taarifa yoyote kuhusu madai hayo. 

Inaonekana kuwa, kutokana na stratijia yake kuu kuhusiana na eneo la Asia, Marekani haitakuwa tayari kuondoa wanajeshi wake wote huko Afghanistan, na iwapo suala hili litakuwa kweli basi suala la kurejea amani nchini humo litaendelea kuwa ndoto kwa miaka mingine kadhaa.    

Tags

Maoni