Jul 06, 2020 11:25 UTC
  • Jaribio la mfumo wa makombora ya kujihami angani ndani ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad

Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad siku ya Jumamosi ulichukua hatua isiyo ya kawaida na kufanyia majaribio mfumo wa makombora ya kujihami ndani ya ubalozi huo.

Marekani imefanyia majaribio na kuzindua mfumo wa patriot wa makombora ya kujihami ndani ya ubalozi wake mjini Baghdad katika hali ambayo jukumu la kudhamini usalama wa ubalozi kwa kawaida huwa mikononi mwa nchi mwenyeji. Hakuna ubalozi wowote wenye haki ya kutumia wanajeshi wake kwa ajili ya kujidhaminia usalama. Kwa mujibu wa kipengele cha pili na ibara ya 22 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 kuhusu haki za kidiplomasia, imebainishwa wazi kuwa jukumu la kulinda usalama wa balozi za kigeni liko mikononi mwa serikali mwenyeji.

Nukta nyingine ni kuwa,  hivi karibuni pia maafisa wa serikali ya Iraq na viongozi wa kisiasa na kidini nchini humo wamekuwa wakikosoa harakati za ubalozi wa Marekani na wanaamini kuwa ubalozi huo haujihusishi na kazi za kidiplomasia kama inavyotakiwa bali jukumu lake kuu ni kazi za kijasusi na kiusalama. Hatahivyo, kama inavyotarajiwa, Wamarekani wamekuwa wakikanusha taarifa hizo.

Hivi sasa, kwa kufanyia majaribio na kuzindia mfumo wa makombora, si tu kuwa ubalozi huo umekiuka mamlaka ya kujitawala ya Iraq bali sasa umebadilika na kuwa kituo cha kijeshi.

Kuhusiana na hili, muungano wa Fat'h wa Iraq katika taarifa, mbali na kulaani kitendo hicho cha ubalozi wa Marekani mjini Baghdad umesema kuwa ubalozi huo sasa umebadilika kutoka kuwa ofisi ya uwakilishi wa kidiplomasia na kuwa kituo cha kijeshi katika kitovu cha mji mkuu wa Iraq. Wairaqi wenye hasira katika mitandao ya kijamii pia sasa wanautaja ubalozi wa Marekani mjini Baghdad kuwa ni kituo cha kijeshi.

Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad

Nukta nyingine ni hii kuwa, ubalozi wa Marekani mjini Baghdad uko katika mtaa unaojulikana kama Eneo la Kijani  au Al-Minṭaqah Al-Haḍrā. Eneo hilo lina balozi kadhaa za kigeni pamoja na idara za serikali na usalama. Kwa msingi huo, kitendo hicho cha Marekani ni tishio kwa balozi zingine ambazo ziko katika eneo hilo na pia ni tishio kwa idara za serikali na usalama za Iraq.

Hatua hiyo ya Marekani imejiri katika wakati huu ambao kunaendelea mazungumzo baina ya Washington na Baghdad kuhusu kuhusu uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Iraq.

Hivi sasa taifa la Iraq linasisitiza kuwa wanajeshi wa Marekani wanapaswa kuondoka nchini humo. Kwa msingi huo, kitendo cha kuzinduliwaa mfumo wa makombora  ndani ya ubalozi wa Marekani ni ishara kuwa, Washington inalenga kujiimarisha kijeshi nchini Iraq nyuma ya pazia la harakai za kidiplomasia ndani ya ubalozi wake mjini Baghdad. Itakumbukwa kuwa mwaka 2011 wakati serikali ya Iraq iliposisitiza kuwa wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo, maelfu ya wanajeshi hao wa Marekani walisalia Iraq lakini kwa vibali vya wanadiplomasia.

Ubalozi wa Marekani umefanyia majaribio na kuzindua mfumo wa makombora ndani ya ubalozi wake kwa kuwa unakabiliwa na vitisho vya usalama.

Katika miezi ya hivi karibuni hisia dhidi ya Marekani zimeongezeka Iraq tokea jeshi la kigaidi la Marekani lilipomuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Naibu Kamanda wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq (Al Hashd al Shabi) Abu Mahdi al Muhandis mapema Januari mwaka huu mjini Baghdad. Tokeo kujiri tukio hilo kumeshuhudiwa ongezeko la vitisho dhidi ya ubalozi na wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.

Watu wa Iraq wanaamini kuwa, kwa upande mmoja Marekani inatumia ardhi ya Iraq kutekeleza hujuma za kigaidi dhidi ya Wairaqi na waitifaki wake na katika upande mwingine haiamini hata kidogo kuwa Iraq ina mamlaka ya kujitawala na uhuru.

Wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Iraq

Takwa kuu la wananchi wa Iraq na makundi mbali mbali nchini humo ni kuondoka mara moja wananchi wa Marekani na kulinda uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi yao.

Tarehe tano Juni 2020, Bunge la Iraq lilipasisha azimio la kutaka wanajeshi wa kigeni waondoke nchini humo. Kwa hivyo  ni wazi kuwa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad umefanyia jaribio na kuzindua mfumo wa makombora ambayo umedai ni kujihami lakini ni wazi kuwa si ya kujihami, bali lengo huu ni kuendelea kukalia kwa mabavu Iraq na kushambulia makundi ya nchi hiyo. Aidha kwa hatua yake hiyo ya Marekani imekiuka wazi mamlaka ya kujitawala Iraq mbali na kuwa kitendo hicho pia kinahesabiwa kuwa ni hujuma na uchokozi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags

Maoni