Jul 07, 2020 07:52 UTC
  • Sisitizo la Uturuki la kutokuwa Saudia na ustahiki wa kushughulikia faili la mauaji ya Khashoggi

Wakati Uturuki inaendelea kufuatilia faili la kesi ya watu waliomuua Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa akiukosoa vikali utawala wa Aal Saud, maafisa wa Ankara wangali wanasisitiza kuwa, serikali ya Saudi Arabia haina ustahiki wa kushughulikia na kuendesha kesi ya Msaudia huyo aliyeuliwa ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki akiwa na umri wa miaka 59.

Fuat Oktay, mshauri wa Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesisitiza kuwa:

Saudi Arabia haina ustahiki wa kuendesha kesi na kuwahukumu wauaji wa Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Aal Saud, ambaye aliuliwa ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo Istanbul.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa Uturuki kuonyesha msimamo mkali kuhusu utaratibu uliotumiwa na Saudia kuendesha kesi ya watu waliomuua Jamal Khashoggi, ambaye alikuwa akiandika makala pia katika gazeti la Washington Post. Kabla ya kauli iliyotolewa na mshauri wa Rais wa Uturuki, serikali ya Ankara iliwahi huko nyuma kutamka pia kwamba, hukumu iliyotolewa na mahakama ya Saudia kuhusiana na mauaji ya Khashoggi haikuwa ya uadilifu na ikataka kuendeshwa kwa uwazi kesi ya watu waliotenda jinai hiyo. Mnamo mwezi Desemba 2019, mahakama moja ya Saudi Arabia ilitoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa watu watano kuhusiana na mauaji ya Jamal Khashoggi na ikawahukumu watu wengine watatu kifungo cha miaka mingi jela kwa kuhusika na mauaji hayo. Hata hivyo hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama ya Saudia iliwatoa hatiani na kuwafutia mashtaka wahusika wawili wakuu wa mauaji hayo.

Fuat Oktay, mshauri wa Rais wa Uturuki 

Mnamo mwezi huohuo wa Desemba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilitoa taarifa maalumu na kutangaza kuwa:

"Uamuzi wa mahakama ya Saudi Arabia haukukidhi hata kidogo matarajio ya jamii ya kimataifa ya kuwekwa wazi masuala yanayohusu mauaji ya Khashoggi na kutendeka haki na uadilifu katika kesi hiyo".

Wakati huohuo kesi ya washtakiwa 20 wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Jamal Khashoggi ilianza kusikilizwa mjini Istanbul, Uturuki siku ya Ijumaa ya tarehe 3 Julai bila washtakiwa wenyewe kuwepo mahakamani. Katika siku hiyo ya mwanzo ya kesi hiyo, Fuat Oktay, mshauri wa Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, ambaye ni shahidi katika kesi hiyo aliashiria katika ushahidi aliotoa mahakamani kuhusu kuhusika moja kwa moja Saud al-Qahtani, mshauri wa zamani wa mahakama ya kifalme na wa masuala ya vyombo vya habari wa Saudia katika mauaji ya Khashoggi na akayanukuu maneno aliyowahi kusema Khashoggi mwenyewe kwamba:

Al-Qahtani alimtisha mtoto mmoja wa Khashoggi na kumtaka amwambie baba yake aache kuukosoa utawala wa Aal-Saud.

Saud al-Qahtani

Hapana shaka kuwa jitihada zilizofanywa na serikali ya Uturuki za kuipa sura ya kimataifa kadhia ya mauaji ya mwandishi huyo wa habari aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud zimepelekea kufichuka mambo kadhaa dhidi ya baadhi ya madola ya kibeberu. Ijapokuwa hadi sasa serikali ya Uturuki bado haijaweza kufikia malengo yake katika kufuatilia mauaji ya Jamal Khashoggi likiwemo la kumweka kitimoto cha kuhusika na mauaji hayo Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, lakini pamoja na hayo inapasa tuseme kuwa, ufuatiliaji uliofanywa na Ankara umewezesha kulipa faili hilo la mauaji sura ya kimataifa. Wakati huohuo mauaji ya Khashoggi yamefichua nafasi ya Marekani na baadhi ya madola mengine makubwa ya dunia katika kuukingia kifua na kuuhami utawala wa Aal Saud mkabala wa kupokea kitita cha fedha kutoka kwa utawala huo. Ukweli ni kwamba mrithi wa ufalme wa Saudia ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa Jamal Khashoggi pamoja na idadi kubwa ya wakosoaji wengine wa utawala wa Riyadh katika miaka kadhaa ya karibuni, lakini uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya madola mengine ya kibeberu ya Magharibi umekwamisha kupandishwa kizimbani mwanasiasa huyo mwanagenzi wa aila ya Aal Saud. Pamoja na hayo, ripota wa Umoja wa Mataifa anayefuatilia hukumu za vifo zinazotekelezwa nje ya utaratibu wa kisheria, alieleza hivi karibuni kuwa, kuna uwezekano wa jina la Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia kujumuishwa kwenye orodha ya watuhumiwa katika faili la mauaji ya Jamal Khashoggi.  Kuhusiana na nukta hiyo, Ekrem Ekşi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Uturuki anasema:

"Mauaji ya Jamal Khashoggi ni sehemu tu ya jinai za ndani zinazofanywa na utawala wa Saudi Arabia; na Aal Saud wanajaribu kutumia kila njia ikiwa ni pamoja na kuwalipa mabilioni ya dola Wamagharibi, ili wajipapatue na kujitua mzigo wa tuhuma hizo."

Jamal Khashogi, anaonekana kwa mara ya mwisho wakati alipoingia ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki

Kwa ujumla inapasa tuseme kuwa: Jitihada na ufuatiliaji uliofanywa na viongozi wa Uturuki umepelekea kuibuka kashfa kubwa iliyouandama utawala wa Aal Saud na baadhi ya madola ya Magharibi hususan Marekani katika uga wa kimataifa. Kutokana na hali hiyo, hapana shaka kuwa, mbali na hatua za utawala wa Aal Saud za kujaribu kuyadogesha mauaji ya Jamal Khashoggi yaliyofanywa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki na kutaka yaonekane jambo lisilo na umuhimu, nchi nyingi za Magharibi na hasa Marekani - ambazo  zinajulikana kuwa ni waungaji mkono wa Saudia kimataifa - nazo pia zimeonyesha na kuthibitisha kivitendo kuwa, hazishughulishwi hata chembe na masuala yanayohusu haki za binadamu.../

Tags

Maoni