Jul 13, 2020 07:31 UTC
  • Wayemen walipiza kisasi kwa kupiga kwa makombora maeneo ya Saudia

Duru za Saudi Arabia mapema leo asubuhi zimetangaza habari ya kusikika sauti za miripuko kadhaa katika maeneo ya Khamis Mushait na Abha ya kusini mwa nchi hiyo.

Duru hizo za Saudia zimetangaza kuwa miripuko hiyo imetokana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni) za jeshi la Yemen na kamati za kujitolea za wanachi wa nchi hiyo.

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Saudi Arabia vimedai kuwa, mfumo wa kujilinda na makombora wa nchi hiyo umekabiliana na mashambulio hayo. Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, droni za Yemen zimeshambulia kambi ya jeshi la anga la Malik Khalid katika eneo la Khamis Mushait katika mkoa wa Asir wa kusini mwa Saudi Arabia. Hadi tunapokea habari hii kulikuwa hakujatolewa taarifa za kina kuhusu mashambulizi hayo na hasara zake.

Droni ya Yemen, Qasif 2

 

Huko nyuma pia jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vilitangaza kuwa, maadamu Saudi Arabia na wenzake wanaendelea kufanya jinai dhidi ya wananchi wa Yemen, basi maeneo yao nyeti na muhimu kama taasisi za uchumi na kijeshi nazo hazitobaki salama.

Siku chache zilizopita pia, mkuu wa timu ya intelijensia ya serikali ya wokovu wa kitaifa ya Yemen alisema kuwa wamekaribia mno kuukomboa mji wa Ma'arib baada ya kuungana na makabila yote ya Yemen.

Abdullah Yahya al-Hakim alisema hayo na kuongeza kuwa, Yemen inao uwezo wa kuvilenge vituo vyote vya mafuta na kiuchumi vya Saudia na kuviangamiza kikamilifu. Aidha amesema, vikosi vya ulinzi vya Yemen vina taarifa nyingi na za kina za sehemu nyeti na muhimu ndani ya ardhi ya Saudi Arabia, Imarati, Tel Aviv na maeneo yaliyo mbali zaidi ya hayo.

Maoni