Aug 02, 2020 06:36 UTC
  • Tathmini ya utendaji wa jeshi la Syria katika kupambana na ugaidi kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuasisiwa kwake

Kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 75 wa kuasisiwa jeshi la Syria, Rais Bashar al Assad amelisifu na kulipongeza jeshi hilo kwa mchango wake katika vipindi tofauti vya vita dhidi ya ugaidi na kuendelea kwake kuwalinda watu wa nchi hiyo.

Jeshi la Syria liliasisiwa tarehe Mosi Agosti mwaka 1945. Kinyume na aghaabu ya majeshi ya nchi za Kiarabu, jeshi la Syria lilishiriki katika vita kadhaa vya kukabiliana na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel, vikiwemo vita vya mwaka 1948, 1967 na 1973. Wakati ambapo majeshi ya baadhi ya nchi zinazojigamba kwa Uarabu hayakuweza kuchukua hatua yoyote kukabiliana na jinai na uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, majeshi ya nchi tatu za Misri, Syria na Jordan yaliingia vitani kupambana na Israel ingawa yalishindwa katika vita hivyo.

Rais Bashar al-Assad akiwa na baadhi ya makamanda wa jeshi 

Tangu mwaka 2011 hadi sasa jeshi la Syria limekuwa kwenye vita vyenye vielezo vipya kabisa, muhimu zaidi kikiwa ni cha kupambana na makundi ya magaidi wanaotoka mataifa kadhaa. Ukweli ni kwamba jeshi la Syria halikuingia vitani kupigana na jeshi la nchi ya kigeni, bali lilipigana vita na makundi ya kigaidi ambayo wapiganaji wao walikuwa raia wa makumi ya mataifa na waliokuwa wakisaidiwa na kuungwa mkono na mhimili wa pande nne za Waarabu, Waebrania, Wamagharibi na Waturuki; lakini pamoja na hayo limepata mafanikio kadhaa muhimu katika vita hivyo vya muda wa takribani miaka 10 sasa.

Moja ya mafanikio hayo muhimu ni kuilinda ardhi yote ya Syria na kuyatimua na kuyatokomeza makundi ya kigaidi katika akthari ya maeneo ya nchi hiyo, nukta ambayo Rais Assad ameitilia mkazo katika salamu zake za pongezi kwa jeshi hilo. Jeshi la Syria halikuwa na tajiriba na uzoefu unaohitajika wakati vilipoanza vita na makundi ya kigaidi kwa sababu makundi hayo ya kigaidi yalikuwa yakitumia mbinu za "wapiganaji wa msituni" ambao huwa hawajipangi kama jeshi rasmi.

Kwa hiyo mbinu yao ya upiganaji na pia utambulisho na uwezo wao wa kupigana vilikuwa tata na visivyoeleweka kwa jeshi la Syria. Lakini kinyume chake, jeshi la Syria lilikuwa na muundo wa jadi wa jeshi, na mbinu zake pia zilikuwa za jadi za upiganaji vita. 

Askari wa jeshi la Syria baada ya kukomboa moja ya maeneo yaliyokuwa yakikaliwa na makundi ya kigaidi

Kwa sababu hiyo, katika miezi ya mwanzoni ya vita hivyo na makundi ya kigaidi, jeshi hilo lilikabiliwa na matatizo kadhaa; na likaonekana kwa kiwango kikubwa kuwa halina uwezo wa kushinda vita hivyo.

Aram Nargiziyan, mtaalamu wa masuala ya kijeshi katika Asia Magharibi ameeleza yafuatayo katika mahojiano na gazeti la Kifaransa la Le Monde, kuhusu hali na udhaifu wa jeshi la Syria mwaka 2012: "Askari wa vikosi vya nchi kavu walikabiliwa na changamoto kubwa. Iliwabidi ama waendane na hali halisi au wafe. Vikosi vikubwa vya jeshi viligawanywa katika vikosi vidogo vidogo ambavyo havikuwa na ufanisi mkubwa kiutendaji. Makamanda waliochoka au waliopoteza sifa kutokana na udhaifu wao waliwekwa kando, wakaja vijana ambao miongoni mwao walikuwemo pia maafisa wanagenzi wenye tajiriba ndogo."

Hata hivyo baada ya kuingia vikosi vya makundi ya muqawama nchini Syria, ambayo yalikuwa na tajiriba ya vita vya msituni na vilevile kutumwa nchini humo washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia kuliliwezesha jeshi la Syria ndani ya muda mfupi kabisa kurejesha nguvu na uwezo wake kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi.

Kielezo muhimu ambacho jeshi la Syria lilikuwa nacho na ndio sababu ya mafanikio liliyopata katika vita vya kupambana na ugaidi ni "uaminifu" wake kwa mfumo wa utawala wa nchi hiyo.

Hapana shaka kuwa sifa ya uaminifu wa jeshi ni moja ya sababu muhimu zaidi za kufanikiwa mfumo wa utawala wa Syria katika kupambana na ugaidi, kwa sababu ndiyo iliyolifanya jeshi hilo liendelee kubaki kwenye medani za mapambano ya kukabiliana na magenge ya kigaidi.

Hayati Meja Jenerali Issam Zahreddine

Wakati huohuo kuwepo makamanda mahiri na wazalendo wenye mapenzi ya nchi kama Meja Jenerali Issam Zahreddine na Meja Jenerali Suheil al-Hassan, ambao walipata mafanikio muhimu ya kistratejia kuliongeza kiwango cha imani ya wananchi na vijana wa Syria kwa jeshi lao na kuwafanya wananchi hao wawe bega kwa bega na jeshi katika kupambana na makundi ya kigaidi.

Hata kama mpaka hivi sasa vita vya kupambana na makundi ya kigaidi vingali vinaendelea nchini Syria, lakini jeshi la nchi hiyo linakabiliwa na changamoto muhimu kadhaa katika zama za baada ya ugaidi. Anton Lavrov amesema katika uchambuzi uliochapishwa na taasisi ya Carnegie ya Marekani kwamba, kuendelea kubakia silaha mikononi mwa baadhi ya makundi yanayobeba silaha na baadhi ya raia na vilevile kuwepo majeshi ya Uturuki na Marekani pamoja na vikosi vya wapiganaji wanaoungwa mkono na nchi hizo katika maeneo ya kaskazini mwa Syria, ndizo changamoto muhimu zaidi zinazolikabili jeshi la nchi hiyo, ambalo kwa namna fulani limeshautathmini na kuuratibu upya muundo wake.../

 

Tags

Maoni