Aug 03, 2020 03:12 UTC
  • Radiamali mbalimbali kwa tarehe ya kuitishwa uchaguzi wa mapema wa Bunge nchini Iraq

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq ameitangaza tarehe 6 Juni ya mwaka ujao wa 2021 kuwa siku ya kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge.

Moja ya vipaumbele muhimu vya Mustafa al-Kadhimi baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Iraq ni kufanyika uchaguzi wa Bunge wa kabla ya wakati. Uchaguzi wa mwisho wa Bunge nchini Iraq ulifanyika mwezi Mei 2018. Hata hivyo maandamano dhidi ya serikali yaliyoanza Oktoba 2019, yalimfanya aliyekuwa Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi ajiuzulu Disemba mwaka huo huo. Serikali ya sasa al-Kadhimi ni ya muda na ina jukumu la kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi wa Bunge na hivyo kuundwa serikali ya kudumu.

Kutangazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi huo wa Bunge kumekabiliwa na radiamali mbalimbali ndani ya Iraq. Moja ya radiamali hizo ni ya Muhammad al-Halbousi, Spika wa Bunge la Iraq ambayo imebeba maana maalumu. Al-Halbousi analalamikia kuainishwa tarehe ya kufanyika uchaguzi huo, kabla ya kupasishwa sheria za uchaguzi na katika radiamali yenye maana maalumu ametaka kufanyika uchaguzi huo kabla hata ya tarehe hiyo iliyotangazwa.

Bunge la Iraq

Majid Shangali, mwanasiasa wa Kikurdi wa Iraq amesema kuhusiana na radiamali ya Spika al-Halbousi kwamba: Ujumbe huo unaonyesha kuwa, al-Halbousi hajaridhishwa na uamuzi wa Waziri Mkuu al-Kadhim wa kuainisha tarehe ya uchaguzi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, radiamali ya al-Halbousi ina maana kwamba, Mustafa al-Kadhimi anataka kulishinikiza Bunge la Iraq. Kwa mujibu wa kipengee cha 64 cha Katiba ya Iraq, Bunge la nchi hiyo litavunjwa kwa kupatikana kura nyingi za ndio za Wabunge ambazo ni theluthi moja ya Wabunge au kwa ombi la Waziri la Waziri Mkuu ambalo litaafikiwa na Rais. Kwa msingi huo, kama uchaguzi utafanyika Juni 6 hapo mwakani, Bunge la Iraq linapaswa kuwa limevunjwa hadi kufikia tarehe hiyo ya kufanyika uchaguzi.

Radiamali nyingine kwa tangazo la tarehe ya uchaguzi wa Bunge wa kabla ya wakati ni kupokelewa kwa mikono miwili tangazo hilo. Baadhi ya makundi, mirengo ya kisiasa na shakhsia mbalimbali wa Iraq wamelipokea pasi na kulikosoa tangazo la kufanyika uchaguzi wa mapema. Hata hivyo baadhi ya shakhsia na mirengo ya kisiasa wamekosoa tarehe hiyo na wametaka kufanyika uchaguzi huo kabla ya Juni mwakani.

Rais wa Iraq Barham Salih

Adnan Fihan, kiongozi wa mrengo wa al-Sadqoun katika Bunge la Iraq amesema kuwa, kufanyika uchaguzi wa mapema Aprili mwakani ni mwafaka zaidi kuliko Juni kwani hadi sasa Iraq inaongozwa na serikali ya muda.

Msimamo wa tatu unahusiana na kipengee cha 64 cha Katiba ya Iraq. Kuhusiana na hili kuna nukta kadhaa kwa upande wa kisheria. Katika kipengee hiki hakujatajwa suala la uchaguzi wa mapema, bali limetajwa suala la uchaguzi kwa sura jumla. Ni kwa msingi huo basi ndio maana Kamisheni ya Sheria ya Bunge la Iraq katika radimali yake kwa tangazo la uchaguzi wa mapema nchini humo lililotolewa na Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi imetangaza kuwa, kiongozi huyo hana haki na ustahiki wa kufanya hivyo.

Nukta nyingine katika kipengee hiki cha 64 cha Katiba ya Iraq ni kwamba, Rais wa nchi anapaswa kuitisha uchaguzi na tarehe ya kufanyika uchaguzi huo inapaswa kuainishwa na Rais. Hii ni katika hali ambayo, hivi sasa tayari Mustafa al-Kadhimi Waziri Mkuu wa Iraq ameshatangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge la nchi hiyo.

Adil Abdul-Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq aliyelazimika kujizulu kufuatia maandamano ya wananchi

Radiamali ya nne inayohusiana na tangazo la kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge ni uungaji mkono wa kufanyika uchaguzi huo. Akthari ya Wairaqi wanaamini kuwa, kufanyika uchaguzi huo kutawafanya wananchi washiriki na hivyo Iraq kuvuka kipindi cha mgogoro wa wananchi kutokuwa na imani na mfumo wa sasa wa kisiasa nchini humo.

Ahmad al-Assad, mmoja wa Wabunge wa Iraq ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Hatua muhimu zaidi katika njia ya mageuzi na kuvuka katika mgogoro wa kutoamianiana uliojitokeza baina ya serikali na wananchi ni kufanyika uchaguzi wa mapema katika mazingira salama na wananchi kushiriki kwa wingi.

Nukta ya mwisho ni hii kwamba, radiamali mbalimbali za kuainishwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge hususan radiamali iliyotolewa na Muhammad al-Halbousi, Spika wa Bunge la Iraq ni ishara ya wazi kwamba, serikali ya Bghdad inakabiliwa na kibarua kigumu katika njia ya kuelekea  uchaguzi na kuna haja ya kuweko irada na azma thabiti na imara zaidi ya kufanyika uchaguzi huo.

Tags

Maoni