Aug 04, 2020 01:30 UTC
  • Shambulio la Israel dhidi ya Gaza; shambulio la tatu dhidi ya muqawama katika kipindi cha wiki mbili

Ndege za kivita za utawala haramu wa Israel Jumatatu alfajiri zilifanya mashambulio katika maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza.

Mashambulio hayo ni ya tatu ya aina hiyo dhidi ya mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Shambulio la kwanza lilitekelezwa tarehe 20 mwezi uliopita wa Julai dhidi ya Syria. Katika shambulio hilo, ndege za kivita za utawala huo zilishambulia viunga vya Damascus, mji mkuu wa Syria na kumuua shahidi Ali Kamil Muhsin, mmoja wa wapiganaji wa chama cha Hizbullah cha nchini Lebanon.

Kufuatia shambulio hilo, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vililinukuu jeshi la Kizayuni likidai kwamba Hizbullah ilikuwa inajiandaa kulipiza kisasi, jambo lililoibua hofu na wasiwasi mkubwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Wasiwasi huo uliupelekea utawala huo kufanya shambulio la pili tarehe 27 Julai, katika miinuko ya Kafr Shouba na mashamba ya Shab'aa ya nchini Lebanon. Kisingizio cha kufanyika shambulio hilo kilisemekana ni kujipenyeza wapiganaji wa Hizbullah ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu. Madai hayo mwanzo yalikanishwa na Hizbullah na hatimaye baada ya kupita masaa 48, Avichay Adraee, msemaji wa jeshi la utawala huo naye akasema kwamba shambulio hilo lilifanyika kimakosa.

Uchokozi wa Israel katika anga ya Syria

Shambulio la tatu la utawala wa kibaguzi wa Israel lilifanyika Jumatatu alfajiri katika Ukanda wa Gaza katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu baada ya kushambuliwa nchi nyingine jirani za Lebano na Syria.

Jeshi la Israel linadai kwamba limetekeleza shambulio la hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza ikiwa ni katika kujibu shambulio la makombora yaliyorushwa na Wapalestina kutokea ukanda huo, madai ambayo yamekanushwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.

Mashambulio hayo kabla ya jambo lolote lile yanathibitisha ukweli kwamba Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala huo ameazimia kuanzisha vurugu na vita dhidi ya mrengo wa mapambano ya Kiislamu kwa ajili ya kukwepa matatizo ya ndani yanayomkali. Baraza lake la mawaziri limeshindwa kabisa kukabiliana na mgogoro wa kuenea virusi vya corona katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu. Matatizo ya kiuchumi ya Wazayuni pia yameongezeka kwa namna ya kutisha katika kipindi hiki kigumu.

Wakati huohuo, mafaili ya ufisadi wa fedha ya Netanyahu yamepuuzwa na kutoshughulikiwa vilivyo na mahakama za utawala huo. Mjumuiko wa masuala hayo umeibua maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa dhidi ya waziri mkuu wa utawala huo, na hivyo kukaribia kumng'oa madarakani.

Kwa msingi huo, Netanyahu ambaye hana matumaini tena ya kupungukiwa na matatizo mengi ya ndani yanayomwandama, ameamua kuanzisha chokochoko na uchokozi dhidi ya mrengo wa mapambano ya Kiislamu ili kuzihadaa fikra za waliowengi ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Israel ikishambulia Ukanda wa Gaza

Fauzi Barhum, Msemaji wa Hamas katika radiamali yake kuhusu mashambulio ya utawala wa kigaidi wa Israel Jumatatu alfahiri, amesema kuwa lengo la utawala huo kufanya mashambulio hayo katika Ukanda wa Gaza ni kuwasukumia watu wa Palestina matatizo na migogoro yake ya ndani ili kuhadaa fikra za waliowengi ulimwenguni kuhusu migogoro ya kisiasa ya Israel.

Ukanda wa Gaza umeshambuliwa katika mazingira ambayo tokea mwaka 2006 ukanda huo uko chini ya mzingiro mkali wa anga, nchi kavu na bahari unaotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel na hivyo kubadilishwa kuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani. Bila shaka mzingiro huo wa kinyama umehatarisha pakubwa maisha ya wakazi wa ukanda huo.

Katika upande wa pili, mashambulizi ya kichokozi ya Israel yamefanyika katika hali ambayo makundi yote ya Palestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yana msimamo mmoja dhidi ya mpango wa ubaguzi wa rangi wa 'Muamala wa Karne' na kuunganishwa ailimia 30 ya ukingo huo na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Inaonekana kuwa utawala huo umefanya shambulio la hivi karibuni ili kulenga umoja huo wa Wapalestina.

Tags

Maoni