Aug 04, 2020 01:32 UTC
  • Imran Khan akosoa mashambulizi ya Saudia huko Yemen, asema yanayofanyika Kashmir ni sawa na jinai za Manazi wa Ujerumani

Waziri Mkuu wa Pakistan amekosoa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya taifa la Yemen.

Imran Khan ameiambia televisheni ya al Jazeera ya Qatar kwamba yanayofanyika nchini Yemen ni maafa ya kibinadamu. 

Ameashiria uharibifu mkubwa uliofanywa na Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen na kusema: Islamabad inafanya jitihada kubwa za kusitisha mashambulizi na vita huko Yemen.

Imran Khan pia amezungumzia maafa ya Waislamu nchini India na kusema yanafanana na yale yaliyofanywa na Manazi wa Ujerumani wakiongozwa na Hitler.

Amesema India imedhibitiwa na aidiolojia kali inayojulikana kama kundi la RRS na kusisitiza kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita jimbo la Kashmir limefungwa kakamilifu na uchumi wake umesambaratishwa baada ya kutumwa wanajeshi laki 8 wa India katika eneo hilo.

Askari wa India wakiwanyanyasa wakazi wa Kashmir.

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema India imeifanya Kashmir kuwa jela kubwa ya wazi na kwamba Islamabad imelijulisha Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu maafa makubwa yanayofanyika katika eneo hilo.

Imran Khan ameyatuhumu madola makubwa kuwa yanatumia siasa za kindumakuwili kuhusiana na Waislamu wa India na wakazi wa jimbo la Kashmir kwa sababu ya maslahi yao ya kiuchumi.

Tags

Maoni