Aug 04, 2020 11:16 UTC
  • Rais wa Iraq aunga mkono kufanyika uchaguzi wa mapema nchini humo

Rais wa Iraq amekaribisha pendekezo la Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mustafa al Kadhimi kuhusu kufanyika mapema uchaguzi wa bunge.

Rais Barhum Salih wa Iraq ameutaja wito wa kuendesha uchaguzi wa bunge wa mapema nchini humo kuwa moja ya masuala ya lazima kwa ajili ya mageuzi ya kisiasa yanayohitajika na ametaka kukamilishwa ratiba za uchaguzi haraka iwezekanavyo na kutumwa ratiba hiyo bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa na kutekelezwa. 

Rais wa Iraq aidha ametaka kuharakishwa kuidhinishwa marekebisho ya sheria yanayohusiana na Mahakama Kuu ya Federali na kuongeza kuwa: Muda wa kuendesha  uchaguzi katika kipindi cha chini ya miezi miwili litafikiriwa rasmi iwapo bunge litavunjwa. 

Mustafa al Kadhimi Waziri Mkuu wa Iraq ametangaza kuwa uchaguzi huo wa mapema ambao ni moja ya majukumu ya serikali yake ya muda utafanyika mwezi Juni mwaka kesho.

Mustafa aI Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq  

Uchaguzi wa mwisho wa bunge wa Iraq ulifanyika Mei 12 mwaka 2018; hata hivyo ulikosolewa kutokana na kuwepo madai ya kuibiwa kura na dosari nyingine zilizojitokeza katika uchaguzi huo.  

Tags