Aug 04, 2020 11:19 UTC
  • Kujiuzulu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon; duru mpya ya ukwamishaji mambo dhidi ya serikali ya Hassan Diab

Nassif Hitti, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon Jumatatu ya jana tarehe 3 Agosti alitangaza kujiuzulu wadhifa huo.

Rais Michel Aoun na Waziri Mkuu Hassan Diab sambamba na kukubali takwa la kujiuzulu Nassif Hitti, walimuarifisha Charbel Wehbe kuwa Waziri mpya wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo. Swali muhimu ni kwamba, kwa nini Nassif Hitti amejiuzulu nafasi yake kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon?

Katika hili kuna mambo matatu:

Jambo la kwanza ni kitu ambacho Nassif Hitti mwenyewe amekieleza. Hitti amedai katika taarifa yake ya kujiuzulu juu ya kutokuweko malengo ya kitaifa na azma njema kwa ajili ya kuleta mageuzi yanayofaa na yanayozingatiwa na jamii ya kimataifa kuwa ndio sababu iliyomsukuma ajiuzulu. Madai hayo yanatolewa katika hali ambayo, njama na ukwamishaji mambo wa nje na wa ndani dhidi ya serikali ya Lebanon zilianza katika siku za awali kabisa za kuanza kazi serikali ya Waziri Mkuu Hassan Diab.

Jambo la pili ni malalamiko ya Nassif Hitti kwa satuwa na ushawishi wa Gebran Bassil, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon aliyetangulia na uingiliaji wake katika utendaji wa Hitti. Gebran Bassil ni kiongozi wa chama cha Harakati Huru ya Kizalendo (Free Patriotic Movement) ambaye alikuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon katika serikali ya Saad Hariri, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

Jambo la tatu ni muamala wa udunishaji na udhalilishaji wa Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa katika safari yake ya hivi karibuni huko nchini Lebanon. Le Drian alifanya safari yake ya siku tatu nchini Lebanon tarehe 22 hadi 24 za mwezi uliopita wa Julai. Katika matamshi yake yaliyokiuka ada za kidiplomasia, Waziri huyo wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa alisema kuwa: Hali ya mambo nchini Lebanon ni ya hatari. Lazima kutekelezwe mageuzi. Huu ni ujumbe wangu niliokuja nao na hili ni takwa la jamii ya kimataifa.

Kuhusiana na jambo hilo, Sayyid Hadi Sayyid Afqahi, mtaalamu na mweledi wa masuala ya Asia Magharibi anaamini kuwa, matamshi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa aliyoyatoa huko Beirut yalikuwa ya udhalilishaji. Hatua ya Nassif Hitti ya kunyamaza na kutomjibu Le Drian ilikabiliwa na radiamali kali ya Hassan Diab, Waziri Mkuu wa Lebanon. Mtaalamu huyo wa masuala ya Asia Magharibi ameongeza kuwa, Nassif Hitti ana mielekeo ya Kifaransa na hakutoa majibu mwafaka kwa muamala ya udhalilishaji wa Jean-Yves Le Drian na kivitendo alipuuza mamlaka ya kujitawala Lebabon.

Kimya hicho cha Nassif Hitti, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon aliyejiuzulu ilikabiliwa na jibu kali la Waziri Mkuu Hassan Diab ambaye alimhutubu kwa kumwambia hapokei amri kutoka kwa mtu. Radiamali hiyo kali ya Diab na sisitizo lake la mamlaka ya kujitawala Lebanon inatajwa kuwa sababu muhimu ya kujiuzulu Nassif Hitti.

Hassan Diab, Waziri Mkuu wa Lebanon

Nukta muhimu ni hii kwamba, kujiuzulu Nassif Hitti kumefanyika kwa lengo la kutoa taathira hasi kwa serikali ya Waziri Mkuu Hassan Diab. Serikali ya Diab ilianza kazi zake Februari mwaka huu katika hali ambayo kwa upande mmoja ilikuwa ikikabiliwa na upinzai mkali wa mrengo wa Kimagharibi ndani ya Lebanon ambao haukushiriki katika kikao cha Bunge cha kupiga kura ya kuwa na imani na serikali yake. Aidha katika upande pili, ilikuwa ikikabiliwa na upinzani wa mhimili wa Kimagharibi kinara wake akiwa Marekani na Ufaransa kama ambavyo Uwaziri Mkuu wake ulikuwa ukikabiliwa na upinzani wa mhimili wa Kiarabu hususan Saudi Arabia na Imarati pamoja na utawala haramu wa Israel.

Katika kipindi cha miezi sita ya umri wa serikali ya Waziri Mkuu Hassan Diab nchini Lebanon, mirengo yenye mielekeo ya Umagharibi ndani ya Lebanon na upinzani wa nje wamefanya njama na ukwamishaji mwingi wa mambo dhidi ya serikali hiyo hata kufikia hatua ya kuandaa mazingira ya kukaribia kuiangusha. Kwa awamu kadhaa Lebanon ilishuhudia maandamano dhidi ya serikali ya Hassan Diab ambapo Waziri Mkuu huyo alitangaza wazi juu ya nafasi na satuwa ya ndani katika maandamano na njama za kuzusha vuruga katika nchi hiyo.

Inaoneana kuwa, hata kujiuzulu Nassif Hitti ni mwendelezo wa njama na kutaka kuikwamisha serikali ya Waziri Mkuu Hassan Diab. Nukta ya mwisho ni hii kwamba, kukubaliwa barua ya kujiuzulu Nassif Hitti na kuarifishwa katika kipindi cha mfupi mno Charbel Wehbe ni jambo linaloonyesa kuwa, Rais Michel Aoun na Waziri Mkuu Hassan Diab walikuwa wamejiandaa tangu kabla kwa ajili ya kukabiliana na senario za wapinzani nchini humo.

Tags

Maoni