Aug 05, 2020 06:32 UTC
  • Lebanon inaomboleza vifo vya watu 100 baada ya mlipuko wa Beirut; mataifa mbalimbali yatoa pole

Taifa la Lebanon linaomboleza baada ya mlipuko mkubwa katika mji mkuu Beirut uliopelekea zaidi ya watu 100 kuuawa na wengine zaidi ya 4000 kujeruhiwa.

Mlipuko huo ulitokea katika ghala nambari 12 la Bandari ya Beirut na kwamba sababu ya moto ni mada za milipuko ambazo zilikuwa zimehifadhiwa hapo.

Mlipuko huo wa jana ulikuwa mkubwa kiasi cha kusikika kilomita nyingi kutoka eneo la tukio. Taarifa zaidi kutoka mji mkuu wa Lebanon Beirut zinasema kuwa, mlipuko huo umesababisha hasara kubwa kwa nyumba za makazi na pia katika idara binafsi na za serikali hasa majengo yaliyokuwa karibu na tukio hilo.

Mataifa mbalimbali yametoa salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Lebanon na kutangaza kuwa pamoja na taifa hilo katika kipindi hiki kigumu hasa kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Wafanyakazi wa zima moto wakijaribu kuzima moto baada ya mlipuko

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pamoja wametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha kwenye matukio hayo huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi. Iran kupitia Waziri wake wa Mashauri ya Kigeni Dakta Muhammad Javad Zarif imetuma salamu za mkono wa pole na za kuliwaza kwa taifa la Lebanon. Aidha Syria, Iraq, na Yemen ni miongoni mwa mataifa yaliyotuma salamu za mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Lebanon. Rais Michel Aoun ameitisha kikao cha dharura leo huku akitangaza hali ya hatari ya wiki mbili nchini humo.

Tags

Maoni