Aug 09, 2020 11:46 UTC
  • Canada yaimarisha ulinzi wa Saad al-Jabri anayesakwa na bin Salman ili auawe

Serikali ya Canada imeimarisha maradufu ulinzi na usalama wa Ali Saad al-Jabri, mkuu wa zamani wa Idara ya Intelijensia la Saudi Arabia ikihofia kuuawa na serikali na Saudi Arabia.

Gazeti la Globe and Mail la Canada limeripoti kuwa, Idara ya Usalama ya nchi hiyo limefichua habari ya kufanyika juhudi mpya za kutaka kumuua Saad al-Jabri na ndio maana serikali ya nchi hiyo imechukua uamuzi wa kuzidisha ulinzi na usalama mahala anapoishi.

Ripoti zinasema kuwa, mahala anapoishi Saad al-Jabri hivi sasa pana ulinzi mkali ambapo mbali na walinzi wake binafsi kuna askari usalama wa serikali ya Canada ambao wamepewa jukumu la kumlinda mkuu huyo wa zamani wa Idara ya Intelijensia la Saudi Arabia.

Wiki iliyopita Saad al-Jabri, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Canada na anayejulikana kama "Kisanduku Cheusi cha Aal Saud" aliwasilisha mashtaka katika mahakama moja ya Marekani akisema kuwa, Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia mwaka 2018 alituma timu ya kumuua, ingawa njama za mauaji hayo zilisambaratishwa na viongozi wa Canada.

Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Kisaudia aliuawa kinyama mwaka 2018 katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Uturuki

Saad al-Jabri ana nyaraka muhimu zinazomhusu mfalme Salman bin Abdul-Aziz pamoja na mwanawe Muhammad bin Salman ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ambapo kama nyaraka hizo zitavuja na kusambazwa zinaweza kuharibu mno haiba ya bin Salman ulimwenguni.

Itakumbukwa kuwa, Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Kisaudia wa gazeti la Washington Post aliuawa kinyama mwaka 2018 kwa amri ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme. Khashoggi aliuawa kikatili katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki na mwili wake kukatwa vipande vipande.

Maoni