Aug 10, 2020 04:26 UTC
  • Radiamali ya Qatar kwa njama ya Saudia ya kupanga kuishambulia kijeshi nchi hiyo

Qatar imejibu taarifa iliyofichuliwa na jarida la Foreign Policy linalochapishwa nchini Marekani kuhusu pendekeo lililotolewa na Saudi Arabia kwa Marekani la kuiomba iishambulie Qatar na kutangaza kuwa kutokanusha suala hilo kunamaanisha kuwa Saudi Arabia ilikuwa kweli na nia ya kuishambulia Qatar.

Mvutano ndani ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi  kati ya Saudi Arabia na Qatar ulianza mwezi Juni mwaka 2017. Saudi Arabia na Qatar pamoja na Kuwait, Oman, Imarati na Bahrain ni nchi wanachama wa baraza hilo. Utawala wa Aal Saud ambao unajikweza mbele ya nchi zingine wanachama wa baraza hilo unataraji kuziona nchi hizo zikiratibu sera zao za nje kwa kufuata matashi yake; suala ambalo  linapingwa waziwazi na Qatar, na kwa sura isiyo ya wazi, na nchi mbili za Kuwait na Oman. 

Mwaka 2017 Saudi Arabia ilitegemea kuwa Qatar  itaunga mkono siasa zake katika eneo zikiwemo sera za kuipiga vita Iran.  Serikali ya Saudia kuanzia mwaka 2015 wakati walipoingia madarakani mfalme Salman bin Abdulaziz na Muhammad bin Salman ilifanya jitihada kubwa za kutaka ionekane kwamba Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni nchi tishio kubwa; suala lililofikia kilele chake katika kikao cha nchi za Kiarabu na Kiislamu kilichofanyika huko Riyadh mwezi Mei mwaka 2017 kwa kuhudhuriwa na Rais Donald Trump wa Marekani. Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani alitamka mara baada ya kumalizika mkutano huo wa Riyadh kuwa Iran ni nchi kubwa na kwamba uhusino wa Qatar na Iran ni mzuri. Amir wa Qatar alisema kuwa "Iran ina umuhimu kwa upande wa kieneo na Kiislamu na jambo hilo haliwezi kupuuzwa."  

Amir wa Qatar, Sheikh Tamim binHamad Al Thani

Katika makala yake iliyochapishwa na jarida la Foreign Affairs mwaka 2017, "Simon Handerson" anasema: sababu kuu ya mvutano katika uhusiano wa Qatar na Saudi Arabia ni aina ya uhusiano uliopo kati ya Qatar na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao hauendani na siasa za Saudi Arabia. Aidha aliandika kuwa: Mtazamo wa Qatar kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepelekea kufeli kwa jitihada za Saudia za kuidhihirisha Iran kuwa ni tishio kupitia Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. 

Hatua ambazo Qatar imekuwa ikitekeleza katika kukabiliana na siasa za Saudi Arabia katika eneo zimekuwa nzito na kuilemea Saudia na kuipelekea nchi hiyo kutoa pendekezo kwa Marekani la kuishambulia Qatar. Jarida la Foreign Policy la nchini Marekani tarehe 6 mwezi huu wa Agosti liliripoti kuwa Mfalme wa Saudi Arabia mwaka 2017 na siku moja baada ya Saudia yenyewe, Imarati, Misiri na Bahrain kuizingira Qatar aliwasiliana kwa simu na Rais Donald Trump wa Marekani na kumpa pendekezo hilo la kuishambulia Qatar; hata hivyo Trump alipinga vikali pendekezo hilo. Gazeti la Wall Street linalochapishwa huko Marekani pia mwezi Mei mwaka jana lilifichua kuwa jeshi la Saudia mwaka 2017 lilipanga kuishambulia Qatar.   

Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia ambaye ana kiu kubwa ya kukalia kiti cha ufalme wa nchi hiyo amefanya juhudi kubwa na kila awezalo kuzidhihirishia fikra za waliowengi huko Saudia kupitia vita kwamba, katika zama za utawala wake akiwa Mfalme, Riyadh itakuwa na nguvu na itakuwa dola la kwanza lenye nguvu Magharibi mwa Asia. Sababu hiyo pia ndyo iliyopelekea kuanzishwa vita mwaka 2015 huko Yemen; na mwaka 2017 pia Riyadh ilikuwa imekusudia kuishambulia kijeshi Qatar. Bin Salman si tu ameshindwa vibaya katika vita dhidi ya Yemen bali kushindwa katika kuanzisha vita dhidi ya Qatar pia kunaonyesha kuwa Saudi Arabia haina ubavu hata wa kupitisha maamuzi katika siasa zake za nje bila ya ruhusa ya Marekani.   

Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia  

Nukta muhimu ni hii kuwa moja ya malengo ya kuasisiwa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi mwaka 1981 ilikuwa ni kuziunga mkono nchi sita wanachama mbele ya uvamizi wa nchi ajinabi. Uamuzi wa Saudia wa kutaka kuishambulia Qatar ambayo ni moja ya wanachama wa Baraza hilo la Ushirikiano unaonyesha kuwa, baraza hilo limepoteza kabisa falsafa ya uwepo wake. Kuhusiana na suala hilo," Ahmad bin Saeed al Rumaihi Mkuu wa Ofisi ya Habari katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ameandika: inashangaza kuona  chaguo la kijeshi linaainishwa na nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi dhidi ya nchi nyingine mwanachama; baraza ambalo asili yake liliasisiwa kwa ajili ya kudhamini "usalama wa pamoja wa kundi zima". 

 

 

 

 

 

Tags

Maoni