Aug 10, 2020 06:28 UTC
  • Uungaji mkono wa wazi wa Marekani kwa hatua za uharibifu nchini Lebanon

Marekani imeshadidisha hatua na mwenendo wake wa uingiliaji masuala ya ndani ya Lebanon kwa shabaha ya kudhoofisha mhimili wa muqawama na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah.

Mlipuko mkubwa uliotokea juma lililopita katika bandari ya Beirut kwa mujibu wa serikali ya Rais Donald Trump imeyapatia fursa nzuri madola ya Magharibi ikiwemo Marekani na Ufaransa ya kuingilia masuala ya ndani ya Lebanon. Ubalozi wa Marekani nchini Lebanon umelitumia tukio hilo la maafa katika bandari ya Beirut lililopelekea makumi ya watu kuuawa na maelefu ya wengine kujeruhiwa kama fursa ya dhahabu na kujionyesha kuwa ni mfuasi wa wananchi na hivyo kutoa matamshi ya kuunga mkono mikusanyiko na maandamano ya wananchi katika mazingira haya nyeti na hatari.

Ubalozi wa Marekani umetoa taarifa kuhusiana na malalamiko na hujuma dhidi ya vituo na idara za serikali mjini Beirut na kudai kwamba, Marekani inatambua haki ya wananchi wa Lebanon ya kuandamana kwa amani na inawataka wananchi wote kujiepusha na vitendo vya utumiaji mabavu. Aidha ubalozi huo umedai kwamba, taifa la Lebanon limeteseka kwa masaibu mengi na kwamba, linastahiki kuwa na viongozi ambao wataruhusu kutolewa madai na kupigania matakwa kwa njia ya wazi kabisa.

Mlipuko mkubwa uliotokea katika bandari ya Beirut Jumanne iliyopita

Msimamo wa kidhahiri wa Marekani wa kuunga mkono malalamiko ya wananchi kwa hakika ni njama za Washington zinazofanyika katika fremu ya kuyaelelekeza malalamiko hayo na kuwa dhidi ya Hizbullah na kiongozi wake Sayyid Hassan Nasrullah. Katika kipindi cha miwili iliyopita, Marekani imefanya njama nyingi za kuleta mbinyo na mashinikizo dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon. Mfano wa wazi ni kuiwekea vikwazo harakati hiyo na kuwashajiisha washirika wake wa Ulaya waungane na Washington katika kutumia wenzo wa kisiasa na kiuchumi dhidi ya Hizbullah. Hususan katika miezi ya hivi karibuni Marekani imetekeleza vikwazo dhidi ya watu na asasi zenye mfungamano na Hizbullah ya Lebanon.

Alexander Zasypkin, balozi wa Russia nchini Lebanon amesema kuwa, inawezekana Washington inatafuta na kufuatilia njia ya kuishinikiza Lebanon kupitia  kuidhoofisha Harakati ya Hizbullah, lakini njia hiyo haina natija nyingine ghairi ya kuzidi kuiimarisha harakati hiyo.

Hivi sasa vyombo vya habari vya Magharibi na baadhi ya mirengo ya kisiasa nchini Lebanon inafanya njama za kuleta mfungamano baina ya mlipuko mkubwa wa Beirut na siasa pamoja na hatua za Harakati ya Hizbullah na kuipaka matope harakati hiyo na kuionyesha kuwa ndio msababishaji wa hali mbaya ya sasa ya nchi hiyo.

Hassan Diab, Waziri Mkuu wa Lebanon

Hii ni katika hali ambayo, hali mbaya ya kiuchumi ya Lebanon inahusiana na siasa pamoja na sera za serikali iliyopita ya nchi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu Saad al-Hariri. Lebanon ilikumbwa na mgogoro wa kiuchumi na kisiasa kuanzia katikati ya mwezi Oktoba mwaka jana (2019).

Mgogoro huo ulianza baada ya Waziri Mkuu wa wakati huo Saad al-Hariri akiwa na lengo la kuokoa uchumi wa nchi hiyo alichukua hatua ya kuongeza ushuru wa baadhi ya bidhaa nchini humo. Baada ya hapo Saad al-Hariri akajizulu na Januari mwaka huu kukaundwa serikali mpya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Hassan Diab. Hata hivyo, mlipuko wa Jumanne iliyopita katika bandari ya Beirut umevuruga zaidi hali ya mambo ya nchi hiyo.

Sambamba na hatua za Marekani zinazofanyika katika fremu ya kushajiisha na kuchochea vurugu, machafuko na kushambulia idara za serikali nchini Lebanon, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa naye ameingilia masuala ya ndani ya Lebanon na amewatishia wazi wazi viongozi wa nchi hiyo ya Kiarabu kuhusiana na kutekeleza matakwa ya Paris. Akiwa katika safari yake mjini Beirut hivi karibuni ambayo kidhahiri ilifanyika kwa lengo la kuchunguza hali mbaya ya mji huo baada ya mlipuko katika bandari ya Beirut alisisitizia ulazima wa kutekelezwa matakwa ya Paris na akatishia kwamba, kinyume na hivyo yeye mwenyewe ataelekea katika nchi hiyo na kufuatilia moja kwa moja matakwa yake.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

George Malbourno, mwandishi wa habari wa Kifaransa amenukuu kutoka kwa duru moja iliyokuweko katika vikao vya Rais wa Ufaransa mjini Beirut na kuandika kwamba, Macron alitishia kwamba, kama hakutafanyika marekebisho, basi baadhi ya viongozi wa nchi hiyo watawekewa vikwazo. Macron alidai kwamba, atazindua mpango unaojulikana kama ‘Ubunifu wa Kisiasa’.

Basheer Nafi, mwanahistoria wa Kiaplestina anayeishi nchini Lebanon ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Macron alitangaza bila aibu yoyote kwamba, yumo mbioni kuainisha mkataba mpya kwa ajili ya uhai wa kisiasa wa Lebanon na katika safari yake fupi katika mji wa Beirut uliokumbwa na msiba, alifanya mambo kama vile Lebanon ingali inakoloniwa na Ufaransa.

Tab’an, ni jambo lililo wazi kwamba, ubunifu wa kisiasa ulioandaliwa na Rais wa Ufaransa, ni njama katika fremu ya kusukuma mbele lengo kuu la Washington ambalo ni kuimarisha nafasi ya mrengo wenye muelekeo wa Kimagharibi nchini Lebanon na wakati huo huo kuwadhoofisha wafuasi wa mhimili wa muqawama na Harakati ya Hizbullah. Hii ni katika hali ambayo, kwa kuzingatia nafasi imara iliyonayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon baina ya wananchi wa nchi hiyo, njama za Wamagharibi za kuidhoofisha harakati hiyo na hatimaye kuiangamiza daima zimekuwa zikifeli na kugonga mwamba.

Tags

Maoni