Aug 10, 2020 09:51 UTC
  • Washington Post: Saudia inaongozwa na mwanamfalme wa makundi ya mauaji

Gazeti la Washington Post la Marekani limefanya ulinganisho baina ya mauaji yaliyofanywa na Saudi Arabia dhidi ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo, Jamal Khashogi, na jaribio la mauaji ya kigaidi lililofanywa na watu wa karibu na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman dhidi ya mkuu wa zamani wa Idara ya Intelijensia la Saudi Arabia, Saad al Jabri na kusema Saudi Arabia inaongozwa na mrithi wa ufalme anayesimamia makundi ya mauti.

Chini ya kichwa cha Habari: “Mrithi wa ufalme anayeongoza makundi ya mauti”, tahariri ya Washington Post imesema kuwa mashtaka yaliyowasilishea na Saad al Jabri katika mahakama ya Washington dhidi ya mrithi wa ufalme wa Saudia yanakumbusha mauaji ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya Jamal Khashoggi.

Limeandika kuwa kesi ya Khashoggi ilikuwa kadhia ya hadaa, mauaji na kukwepa adhabu; na hadi sasa maiti ya Khashoggi aliyeuawa na maajenti wa mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman, ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul bado haijapatikana. Tahariri ya Washington Post imeashiria kwamba ukurasa huu mpya wa mauaji ya kigaidi unawashtua wanadamu na kuwakumbusha kwamba, Saudi Arabia inaongozwa na dhalimu asiye na huruma.

Tahariri ya Washington Post imemalizia kwa kusema kuwa, iwapo mashtaka yaliyowasilishwa na Saad al Jabri yatathibitishwa mahakamani basi yatatia nguvu ukweli kwamba, Saudi Arabia inaongozwa na mithi wa ufalme anayesimamia magenge ya mauaji na mauti na anaendelea kukwepa mkono wa sheria kwa mauaji yake.

Wiki iliyopita Saad al-Jabri, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Canada na anayejulikana kama "Kisanduku Cheusi cha Aal Saud" aliwasilisha mashtaka katika mahakama ya Marekani akisema kuwa, Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, mwaka 2018 alituma timu ya kumuua, ingawa njama za mauaji hayo zilisambaratishwa na viongozi wa Canada.

Saad al-Jabri ana nyaraka muhimu zinazomhusu mfalme Salman bin Abdul-Aziz pamoja na mwanawe Muhammad bin Salman ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ambapo kama nyaraka hizo zitavuja na kusambazwa zinaweza kuharibu mno haiba ya bin Salman ulimwenguni.

Al Jabri na mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman

Itakumbukwa kuwa, Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Kisaudia wa gazeti la Washington Post aliuawa kinyama mwaka 2018 kwa amri ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme. Khashoggi aliuawa kikatili katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki na mwili wake kukatwa vipande vipande.

Tags

Maoni