Aug 10, 2020 14:54 UTC
  • Mawaziri wanne na wabunge tisa wa Lebanon wajiuzulu

Mawaziri wanne na wabunge tisa wa Lebanon wamejiuzulu nyadhifa zao kufuatia mlipuko mkubwa ulioikumba nchi hiyo wiki iliyopita.

Marie Claude Najm Waziri wa Sheria, Manal Abdel Samad Waziri wa Habari, Waziri wa Mazingira Damianos Kattar na Waziri wa Fedha wa Lebanon Ghazi Wazni wamejiuzulu nyadhifa zao.

Huku hayo yakiripotiwa viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wameahidi kuipatia Lebanon msaada wa dola milioni 300 baada ya maafa ya Jumanne iliyopita yaliyosababishwa na mlipuko wa bandari ya Beirut. Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wamehudhuria mkutano wa wafadhili ulioongozwa na Ufaransa na Umoja wa Mataifa kufuatia mlipuko mkubwa ulioitokea katika bandari ya Beirut Jumanne iliyopita na kuahidi kuipatia Lebanon dola milioni 300 kama msaada wa kibinadamu kwa ajili ya wananchi.  

Mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut, Lebanon 

Katika taarifa yake, Waziri wa Habari wa Lebanion Manal Abdel Samad amesema anajiuzulu kwa heshima ya waliopoteza maisha, waliojeruhiwa na ambao hawajulikani walipo. Ameongeza kuwa amefanya hivyo kuitikia wito wa wananchi wa kufanyika mabadiliko. Wataalamu wanakadiria kuwa mlipuko huo umesababisha hasara ya takribani dola bilioni 15.  

Maafisa wa serikali ya Lebanon tayari wameanzisha uchunguzi kuhusu mlipuko huo mkubwa uliotokea jioni ya Jumanne iliyopita katika bandari ya Beirut na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 157. Watu wengine zaidi ya elfu tano wamejeruhiwa.

Tags

Maoni