Aug 11, 2020 03:37 UTC
  • Waziri Mkuu wa Lebanon ajiuzulu

Waziri Mkuu wa Lebanon Hassan Diyab amejiuzulu. Diyab amechukua uamuzi huo kufuatia mripuko uliotokea hivi karibuni katika bandari ya Beirut na kutokana na mashinikizo ambayo yameendelea kuiandama serikali ya nchi hiyo.

Katika hotuba kwa taifa aliyotoa kwa njia ya televisheni, Waziri Mkuu wa Lebanon amewahutubu wananchi kwamba, muundo wa ufisadi ulioko nchini humo ni mkubwa zaidi kuliko serikali na balaa la mripuko wa bandari ya Beirut, nalo pia limetokana na ufisadi mkubwa uliopo.

Diyab amesema: "Baadhi ya watu wanapigania kupata ushindi wa kisiasa tu na kusema maneno ya kupendeza watu na wametumia kila kitu kwa ajili ya kuikosoa serikali; hata hivyo lililo muhimu kwetu sisi ni kuiokoa nchi."

Waziri Mkuu wa Lebanon ameongeza kuwa, janga kubwa limetokea Lebanon na inapasa makundi na mirengo yote ishirikiane kwa ajili ya kuivusha nchi na msiba na janga hilo.

Mripuko wa bandari ya Beirut

Hadi sasa watu wapatao 200 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine zaidi ya elfu tano wamejeruhiwa kufuatia miripuko miwili iliyotokea jioni ya Jumanne iliyopita katika bandari ya Beirut kwenye maghala yaliyokuwa yamehifadhi shehena ya tani 2,500 za mada za amoniamu naitreti.

Mripuko wa bandari ya Beirut ulishadidisha mashinikizo dhidi ya serikali ya Hassan Diyab, na kufuatia kujiuzulu mawaziri wanne wa serikali yake, hatimaye Waziri Mkuu huyo naye pia amechukua uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wake huo.

Leo Bunge la Lebanon linatazamiwa kufanya kikao; na hadi itakapoundwa serikali mpya, serikali iliyojiuzulu ya Hassan Diyab itaendelea kufanya kazi kama serikali ya mshikizo.../ 

Tags