Aug 13, 2020 13:58 UTC
  • Bunge la Lebanon laidhinisha sheria ya Hali ya Hatari Beirut, lalipa jeshi mamlaka maalumu

Bunge la Lebanon limeidhinisha utekelezaji wa sheria ya hali ya hatari katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut kufuatia tukio la mripuko katika bandari ya Beirut uliosababisha hasara kubwa ya mali na roho za watu.

Katika kikao kilichofanyika leo kikiongozwa na Spika Nabih Berri, bunge hilo limetangaza kuwa, kuna baadhi ya misamaha itatolewa kwa familia za waathirika wa mripuko wa Beirut.

Spika wa Bunge la Lebanon ameeleza kwamba, bunge hilo limekubali pia uamuzi uliochukuliwa na wabunge saba wa kujiuzulu nyadhifa zao za ubunge.

Kuhusiana na maandamano ya malalamiko yaliyoibuka tena hivi karibuni nchini humo, Berri amesema, jeshi la Lebanon ni miongoni mwa nembo za umoja na uletaji utulivu nchini humo.

Nabih Berri

Tarehe 5 Agosti, siku moja baada ya kutokea mripuko katika bandari ya Beirut, serikali ya Lebanon ilitangaza hali ya hatari kwa kipindi cha wiki mbili, uamuzi ambao umeidhinishwa rasmi kisheria na bunge la nchi hiyo katika kikao chake cha leo.

Sheria hiyo ya hali ya hatari inalipa mamlaka jeshi ya kudhibiti mikusanyiko, vyombo vya habari na hata kuweza kuingia majumbani na kumtia nguvuni mtu yeyote atakayeonekana kuwa ni tishio kwa usalama.

Jumanne jioni ya tarehe 4 Agosti miripuko miwili ilitokea katika bandari ya Beirut kwenye maghala yaliyokuwa yamehifadhi shehena ya tani 2,500 za mada za amoniamu naitreti. Miripuko hiyo imesababisha vifo vya watu wasiopungua 200 na kujeruhi wengine wapatao 6,000.../

Tags

Maoni