Aug 14, 2020 02:53 UTC
  • Ukosoaji wa Rais wa Syria kwa sera za Marekani, Uturuki na Utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi yake

Rais Bashar al Assad wa Syria amekosoa sera za Marekani, Uturuki na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nchi yake na kuitaja sheria ya Marekani ya Caesar kuwa ni "Uharamia wa Baharini".

Rais wa Syria aliyasema hayo siku ya Jumatano katika hotuba aliyotoa kwenye kikao cha ufunguzi wa bunge la nchi hiyo.

Hotuba ya Rais Assad ilikuwa na nukta muhimu kadhaa.

Nukta ya kwanza ni kuhusu ukosoaji wake kwa sera za Marekani kuhusiana na Syria. Marekani ni mmoja wa wapinzani wa mfumo wa utawala wa sasa wa Syria, ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita imechukua hatua kadha wa kadha kwa lengo la kuuangusha mfumo wa utawala wa nchi hiyo.

Rais Bashar al Assad wa Syria akihutubia bunge

Moja ya hatua kubwa na muhimu iliyochukuliwa na Washington katika uga huo ni kuunga mkono ugaidi, ambapo kwa kutumia kipimo cha kuwagawanya magaidi kati ya "wazuri" na "wabaya", imewaunga mkono wale iliowaita magadi 'wazuri' na kuwatumia kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Syria. Kwa mtazamo wa Rais wa Syria, Marekani ina utegemezi kwa makundi ya kigaidi katika siasa zake za nje, kiasi kwamba inaliunga mkono hata kundi la DAESH (ISIS) ambalo inalitaja kama kundi la magaidi wabaya.

Hatu nyingine iliyochukua Marekani dhidi ya mfumo wa utawala wa Syria ni kuiwekea nchi hiyo vikwazo vikali. Serikali ya Marekani inatumia silaha ya vikwazo kwa lengo la kuwashinikiza na kuwalazimisha wananchi wasimame dhidi ya mfumo unaotawala katika nchi yao. Washington ilianza kutumia mkakati wa vikwazo katika miaka ileile ya mwanzoni mwa mgogoro wa Syria, lakini hivi karibuni imeshadidisha kwa kiwango cha juu zaidi vikwazo dhidi ya nchi hiyo kwa kutekeleza sheria iliyoipa jina la Caesar.

Magaidi wa DAESH (ISIS) katika ardhi ya Syria

Rais wa Syria ameitaja sheria ya Caesar kama awamu mpya ya utoaji mashinikizo makali zaidi dhidi ya nchi yake na akasema, vikwazo hivyo havitenganiki na hatua zingine za Marekani dhidi ya Syria, na kwamba kila pale Washington inapokuwa imeshindwa kufikia malengo yake huwa inatumia silaha ya vikwazo. Assad ameufananisha utumizi wa vikwazo unaofanywa na Marekani na mbinu iliyokuwa ikitumiwa hapo zamani na maharamia wa baharini.

Mada nyingine muhimu katika hotuba ya siku ya Jumatano ya Bashar al Assad ilikuwa ni ya ukosoaji wake kwa hatua za Uturuki dhidi ya Syria. Uturuki ni moja ya nchi za eneo, ambayo hapo mwanzo, na katika kuwa bega kwa bega na sera za Marekani, ilipigania kuuangusha mfumo wa utawala wa Syria, lakini baada ya kugonga mwamba na kushindwa kufikia lengo hilo ikaamua kutekeleza sera za kuunga mkono magaidi na kuvamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya ardhi ya nchi hiyo.

Katika ukosoaji wake kwa hatua za Uturuki nchini Syria, Bashar al Assad amesema, hatua za Utruuki ni sawa na za utawala wa Kizayuni, na kwamba katika baadhi ya masuala ni vigumu kupambanua na kutafautisha kati ya "adui Mzayuni" na "Uturuki inayojifanya kuwa na mielekeo ya Ikhwanul Muslimin".

Mada muhimu ya tatu katika hotuba ya rais wa Syria ni kauli yake ya kulaani hatua za utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi yake. Mbali na kuiandama Syria kwa hujuma na mashambulio ya mara kwa mara ya kijeshi, utawala wa Kizayuni wa Israel ukisaidiwa na kuungwa mkono na Marekani unafanya juu chini kuhakikisha unalimega eneo la miinuko ya Golan la Syria na kuliunganisha na ardhi za Palestina unayoikalia kwa mabavu.

Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni

Kuhusiana na nukta hiyo, Assad amesisitiza kuwa, mamlaka ya udhibiti wa miiunuko ya Golan yatarejea mikononi mwa Syria na wala eneo hilo halitaweza kutenganishwa na ardhi ya nchi hiyo.

Nukta muhimu ya kuzingatiwa hapa kuhusu hotuba aliyotoa Rais wa Syria mbele ya bunge la nchi hiyo ni kwamba, mbalii na kutilia mkazo kuendelezwa vita dhidi ya ugaidi na makundi ya kigaidi, amesisitiza pia juu ya ulazima wa bunge kulipa uzito mkubwa suala la utungaji sheria na vilevile serikali kuazimia kwa dhati kupambana na ufisadi na kuboreshja hali za maisha na huduma za afya kwa wananchi, ikiwemo kukabiliana na usambaaji wa virusi vya corona.

Kuzungumziwa masuala yote hayo na Rais wa Syria kunadhihirisha jinsi mfumo tawala wa nchi hiyo unavyojiamini kikamilifu na vilevile ni ithibati ya kurejea uthabiti wa kisiasa na kiusalama nchini humo.../

Tags

Maoni