Aug 14, 2020 08:59 UTC
  • Mapatano ya aibu na usaliti kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni

Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati, utawala ghasibu wa Israel na Marekani zimetoa taarifa ya pamoja zikitangaza kwamba Imarati na utawala haramu wa Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yazo.

Mapatano hayo yanapaswa kutathminiwa katika mitazamo kadhaa.

Mtazamo wa kwanza unahusiana na wakati wa kufikiwa mapatano yenyewe. Imarati sio nchi ya kwanza ya Kiarabu kufikia mapatano kama hayo na utawala ghasibu wa Israel. Misri ilifanya mapatano kama hayo na utawala huo wa Kizayuni mwaka 1978 kupitia mapatano ya Camp David nayo Jordan ikatia saini mapatano kama hayo mwaka 1994 kwa jina la Mapatano ya Wadi Araba ambapo hivi sasa mabalozi wa utawala huo ghasibu wako katika miji mikuu ya nchi mbili hizo za Kiarabu. Misri ilitia saini mapatano ya amani na utawala wa Israel katika kipindi ambacho nchi za Kiarabu zilikuwa zimeshiriki na kushindwa vita vinne na utawala wa Israel na wala hazikuwa na matumaini ya kuushinda wala kuudhoofisha utawala huo. Kwa maneno mengine ni kuwa, Misri ililazimika kutia saini mapatano ya amani na Israel kutokana na udhaifu iliyokuwa nao.

Kinyume na ilivyokuwa katika kipindi hicho, hivi sasa jeshi la utawala wa Kizayuni limedhoofika sana na limekuwa likishindwa mara kwa mara na wapiganaji wa mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika nchi za Lebanon na Palestina. Nukta nyingine ni kwamba mapatano ya Imarati na utawala wa Kizayuni yamefikiwa katika mazingira ambayo hiki ni kipindi cha maadhimisho ya ushindi wa mapambano ya Kiislamu dhidi ya utawala huo ghasibu katika vita vya siku 33 ambavyo vilipiganwa mwaka 2006. Wakati huo huo, utawala wa Israel hivi sasa unapitia kipindi kigumu katika historia yake ya miaka 72 ambapo unashuhudia maandamano ya maelfu ya Wazayuni wanaoandamana kila siku kulalamikia hali mbaya ya maisha inayotokana na uongozi mbovu wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu.

Benjamin Netanyahu (kushoto), Waziri Mkuu wa Israel na Mohammed bin Zayed Al Nahyan Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi

Mtazamo wa pili ni kuhusu iwapo kuna chochote kilichopatikana kwa maslahi ya Imatarati katika mapatano hayo. Mapatano ya Camp David, Wadi Araba na hata mapatano ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni, yalidaiwa kuwa ya amani mkabala na ardhi, yaani Wapalestina walitakiwa kupewa baadhi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel mkabala wa mapatano hayo. Lakini katika mazingira ya sasa hakuna ardhi yoyote itakayopewa Wapalestina bali mipango ya kughusubu ardhi zao na kuziunganisha na zile zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni haijafutiliwa mbali bali imesimamishwa kwa muda tu. Kuhusu ukweli huo mchungu Netanyahu anasema: 'Ninafungamana kikamilifu na mpango wa kuunganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kamwe sitalegeza msimamo kuhusu jambo hilo. Tayari Rais Trump ametambua rasmi vitongoji vya Israel katika Ukingo huo. Sijaakhirisha mpango wowote bali ni Trump ndiye alitaka kuakhirishwa mpango huo. Hata David Friedman, balozi wa Marekani Israel amesisitiza kwamba mpango wa kuunganishwa Ukingo wa Magharibi haujafutiliwa mbali bali umeakhirishwa tu.'

Ni kwa kutilia maanani ukweli huo mchungu ndipo Sayyid Hadi Burhani, mtaalamu wa masuala ya Palestina akasema kwamba mapatano ya hivi karibuni ya Imarati na utawala ghasibu wa Israel ni 'mapatano ya amani mkabala na sifuri bilashi.'

Mtazamo wa tatu ni kwamba mapatano hayo yamefikiwa katika fremu pana zaidi ya mapatano ya 'Maumala wa Karne.' Kinyume na vilivyojaribu kuakisi mapatano hayo baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu mara tu baada kutangazwa na pande husika, ukweli wa mambo ni kuwa mpango wa 'Muamala wa Karne' haujafutwa bali mapatano hayo yamefikiwa katika kalibu ya mpango huo wa ubaguzi wa rangi uliopendekezwa na Marekani. Suala la kufanywa kuwa wa kawaida uhusiano wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni, ndio kitovu na moyo wa mpango huo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali mapatano hayo ya kisaliti

Kwa msingi huo hatua iliyochukuliwa karibuni hivi na Imarati ya kuboresha uhusiano wake na utawala haramu wa Israel bila shaka itazifanya nchi nyingine za Kiarabu kama vile Bahrain kutaka kuwa na uhusiano kama huo na utawala huo wa Kizayuni. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo chombo kimoja cha utawala huo ghasibu kikasema kupitia mahojiano na kanali ya 11 ya televisheni ya Israel kwamba Bahrain itakuwa nchi ya pili kuboreshga uhusiano wake na Israel.

Mtazamo wa nne ni kuwa hata kama kabla ya hapo pia suala la Palestina na Uarabu lilikuwa halipewi umuhimu mkubwa katika siasa za nje za nchi za Kiarabu, lakini mapatano ya hivi karibuni ya Imarati na utawala wa Kizayuni yamethibitisha wazi kwamba suala hilo limefutwa kabisa katika siasa hizo. Pande mbili hizo zimeafikiana kuboresha uhusiano wao katika hali ambayo kufuatia kuzinduliwa mpango wa Mapatano ya Karne na Rais Trump wa Marekani hapo tarehe 28 Januari mwaka mwaka huu, utawala wa Kizayuni ulizidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina wasio na mtu wa kuwatetea. Imarati si tu kwamba haijachukua hatua yoyote ya kuwatetea Wapalestina mbele ya jinai hizo za Wazayuni bali kama anavyosema Saib Arikat (Ereiqat), Katibu wa Kamati ya Utendaji ya PLO, imekuwa ikituza na kuupa zawadi nono utawala huo wa kibaguzi kutokana na jinai zake hizo za kutisha dhidi ya Wapaestina.

Tags

Maoni