Aug 14, 2020 09:34 UTC
  • Palestina yamrejesha nyumbani balozi wake Abu Dhabi baada ya Imarati kuanzisha uhusiano na Israel

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametangaza kuwa balozi wa Palestina mjini Abu Dhabi ameitwa nyumbani kulalamikia hatua ya Imarati ya kuanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.

Riyad al Maliki amesema balozi wa Palestina nchini Imarati ametakiwa kurudi nyumbani haraka iwezekanavyo. 
Awali Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alikuwa amefanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Masuala ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS), Ismail Haniyeh ambapo pande hizo mbili zimetangaza upinzani wao mkubwa dhidi ya mapatano ya Imarati na utawala haramu wa Israel ya kuanzisha uhusiano baina ya pande hizo mbili. 
Mahmoud Abbas amesema kuwa, matabaka yote ya taifa la Palestina yanasimama katika safu moja kupinga hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel au kuutambua rasmi utawala huo kwa gharama ya kukanyaga haki za taifa la Palestina.
Abbas na Haniyeh pia wamesisitiza kuwa, nchi au upande wowote hauruhusiwi kuifanya Palestina, Quds, Msikiti wa al Aqsa na mashahidi wa Palestina kuwa daraja la kuanzishia uhusiano na adui Mzayuni. 

PLO: Imarati imewasaliti Wapalestina

Kwa upande wake Ismail Haniyeh, kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amelaani vikali mapatano hayo yaliyofikiwa baina ya Marekani, utawala haramu wa Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu. Ameongeza kuwa,  Wapalestina wote wanaafikiana na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuhusu kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu (Jerusalem). Haniyeh amepinga vikali hatua yoyote ambayo inafuta haki za Wapalestina na inayokiuka maazimio ya kimataifa. 
Wakati huo huu Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palesina (PLO) Saeb Erekat amemtaka Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit kutoa taarifa inayolaani hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel au ajiuzulu nafasi hiyo.  
Saeb Erekat amesema hatua ya Imarati ni usaliti mkubwa na ni sawa na kulidunga kisu mgongoni taifa la Palestina. Erekat amesema Palestina na Quds ni muhimu zaidi kuliko miji mikuu yote ya nchi za Kiarabu na ya dunia nzima.
Alhamisi ya jana Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili. Hatua hiyo imelaaniwa na harakati zote za mapambano ya ukombozi wa Palestina. 

Tags

Maoni