Aug 25, 2020 11:49 UTC
  • Mkumi ya maelfu ya askari wa Iraq kushiriki katika ulinzi wa maombolezo ya Ashura

Mkuu wa Jeshi la Polisi la Karbala Iraq amesema, askari 30 elfu wamewekwa tayari kwa ajili ya kulinda usalama wa wafanya ziara na waombolezaji wa Ashura ya Imam Husain AS.

Mtandao wa "al Akhbar al Iraq" umemnukuu Ahmed Zweini, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Karbala akisema, askari kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na ile ya Ulinzi wameandaliwa tayari kwa ajili ya kulinda usalama wa wafanya ziara wakati wa maomboleza ya Ashura ya Imam Husain AS.

Kwa upande wake, Majid al Maliki, mjumbe wa Baraza la Mkoa wa Karbala  ametangaza habari ya kuandaliwa mazingira mazuri ya kufanyika kwa hamasa na ufanisi mkubwa maombolezo ya Ashura ya Imam Husain AS na kuongeza kuwa, kila kitu kiko chini ya udhibiti mzuri na hakuna wasiwasi wowote wa kujipenyeza magaidi kwenye maombolezo hayo.

Jeshi la Iraq

 

Jumamosi ijayo ni mwezi 9 Muharram ambayo inajulikana kwa jina maarufu la Tasua na Jumapili ijayo ni mwezi 10 Muharram ambayo inajulikana kwa jina maarufu la Ashura kwa mwaka huu wa 1442 siku hizo tukufu zitasadifiana na tarehe 29 na 30 Agosti, 2020. Magenge ya kigaidi muda wote yanafanya njama za kukwamisha maombolezo ya siku hizo mbili.

Kila mwaka waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali ya Iraq na nje ya Iraq hukusanyika mjini Karbala kutukuza siku hizo mbili kwa ufanisi mkubwa.

Imam Husain AS, Mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW aliuliwa kikatili, kinyama na kidhulma mwezi 10 Muharram mwaka 61 Hijria katika jangwa la Karbala na kufanikiwa kulinda uwepo wa Uislamu kwa kumwaga damu yake toharifu. Tangu mwaka huo hadi leo hii, wapenzi wa kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW huitukuza siku hiyo kwa huzuni na maombolezo licha ya kuweko njama kubwa za kujaribu kusahaulisha tukio hilo chungu.

Tags