Aug 27, 2020 10:54 UTC
  • Iraq yatoa msimamo rasmi kuhusu mapatano ya UAE na utawala wa Kizayuni wa Israel

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuhusu mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu UAE na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwamba, hilo ni suala la ndani linalozihusu pande hizo mbili.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Ahmad Mulla Talal, msemaji wa Waziri Mkuu wa Iraq amesema: Sheria za Iraq zinapiga marufuku kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel; na wakati Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi alipohutubia kikao cha pande tatu kilichofanyika hivi karibuni katika mji mkuu wa Jordan, Amman alisisitiza kuhusu umuhimu wa kadhia ya Palestina. 

Ahmad Mulla Talal

Tangu yalipotangazwa mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Abu Dhabi na Tel Aviv tarehe 13 ya mwezi huu wa Agosti, shakhsia wengi wa kisiasa, wawakilishi na vyama vya siasa vya Iraq wamelaani vikali mapatano hayo.

Hatua hiyo ya Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni imekosolewa na kulaaniwa vikali pia na nchi nyingi za Kiislamu pamoja na makundi ya muqawama na ukombozi wa Palestina.../

 

Tags