Aug 29, 2020 02:35 UTC
  • Sababu za kuchelewa kutangazwa Waziri Mkuu mpya wa Lebanon na changamoto zake

Licha ya kupita siku 19 tangu kujiuzulu Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab, bado hadi hivi sasa hakuna mtu mwingine yeyote aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo nchini humo.

Tarehe 4 mwezi huu wa Agosti kulitokea mripuko mkubwa mjini Beirut Lebanon na kuua watu 177 na kujeruhi zaidi ya watu elfu saba wengine. Baada ya mripuko huo, kulizuka maandamano ya kupinga serikali katika maeneo tofauti ya Lebanon ikiwemo Beirut, maandamano ya fujo ambayo yalijeruhi watu kadhaa na kulazimisha polisi kuingilia. Matokeo yake ni kwamba Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab aliamua kujiuzulu na maandamano yakaisha. 

Diab amekuwa muhaga wa maandamano ya wananchi katika hali ambayo alikuwa amepitisha miezi saba tu madarakani na baraza lake la mawaziri halikuhusika kivyovyote vile na matatizo mbalimbali ya wananchi yakiwemo ya kiuchumi. Hivi sasa Rais Michel Aoun wa Lebanon ametumia haki yake ya kikatiba kumtaka Hassan Diab aendelee kushika nafasi ya Waziri Mkuu hadi atakapochaguliwa mtu mwingine kushika nafasi hiyo.

Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Beri

 

Baada ya siku 19 tangu alipojiuzulu Hassan Diab, sasa taarifa zinasema kuwa, Rais Michel Aoun amekubaliana na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Beri kwamba kuanzia Jumatatu, uanze mchakato wa kuchagua waziri mkuu mpya. Hii ina maana kwamba hadi hivi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa za kuchagua waziri mkuu mpya wa Lebanon. Swali linalojitokeza hapa ni kwamba ni sababu gani zilizopelekea hadi hivi sasa kutoanza mchakato wa kuchaguliwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo na kuna changamoto gani zinazolikabili suala hilo?

Inaonekana kwamba moja ya sababu za kuchelewa mchakato huo katika bunge la nchi hiyo ni hukumu ya Mahakama Maalumu ya Kimataifa ya mauaji ya Rafiq Hariri, Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon. Baada ya kupita miaka 11 hatimaye mahakama hiyo ilitoa hukumu yake tarehe 19 mwezi huu wa Agosti na kutangaza kuwa si Syria wala Hizbullah, hakuna yeyote kati ya hao wawili aliyehusika na mauaji hayo. 

Hukumu hiyo ilitolewa siku tisa baada ya kujiuzulu Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab. Hivyo makundi ya kisiasa ya Lebanon yalikuwa yanasubiri zipite siku 9 hadi utolewe uamuzi wa mahakama hiyo. Katika upande wa pili pia, baada ya kutolewa hukumu hiyo, ilibidi kusubiriwe radiamali na hisia zitakazojitokeza kuhusu uamuzi huo wa mahakama ya kimataifa.

Gazeti la Saudia la al Sharq al Awsat limeandika: Kuchelewa mchakato wa kuchaguliwa waziri mkuu mpya wa Lebanon kuna mfungamano wa moja kwa moja na udharura wa kusahau changamoto zilizojitokeza za baada ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya mauaji ya Rafiq al Hariri, Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

 

Sababu nyingine inaonekana ni mielekeo ya kisiasa inayotawala Lebanon. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Katiba, Waziri Mkuu wa Lebanon lazima atoke miongoni mwa Waislamu wa Kisuni. Lakini waziri mkuu huyo lazima apate kura za wabunge. Kuna majina mbalimbali yametangazwa kushika nafasi hiyo lakini yote hayo yanatokana na propaganda za vyombo vya habari isipokuwa lile lililopendekezwa na Spika Nabih Beri. 

Ikumbukwe kuwa, Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Beri ametangaza rasmi kwamba anamtaka saad Hariri kuwa tena Waziri Mkuu wa Lebanon. Hata hivyo gazeti la al Anbaa la Kuwait limeandika kwamba, kuna mirengo muhimu ya Waislamu wa Kisuni nchini Lebanon ambayo haitaki Saad Hariri awe tena Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Sababu ya tatu ya kuchelewa mchakato wa kuchaguliwa waziri mkuu mpya wa Lebanon ni madola ya kigeni yenye taathira katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Kuna maadui wa kambi ya muqawama kama vile Marekani, Ufaransa na Saudi Arabia ambao wanakwamisha jitihada za kuweza Walebanon kujiamulia wenyewe kwa uhuru masuala yao. 

Amma kinachozingatiwa zaidi na Rais Michel Aoun na Spika Nabih Beri ni uwezo wa Waziri Mkuu mpya wa kuweza kuunda Baraza la Mawaziri na serikali imara ambayo itajumuisha asilimia kubwa ya mirengo na makundi ya kisiasa ya Lebanon. Ikumbukwe kuwa kuwepo ombwe la utawala nchini Lebanon ni katika mambo yanayowafurahisha sana maadui wa taifa hilo, hasa utawala pandikizi wa Kizayuni uliopachikwa jina bandia la Israel.

Tags