Aug 29, 2020 06:32 UTC
  • Askari wa Saudia waingia katika kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Syria

Saudi Arabia imetuma makumi ya wanajeshi wake katika kambi ya kijeshi ya Marekani katika mkoa wenye utajiri wa mafuta wa Hasakah, huko kaskazini mashariki mwa Syria. Hayo yameripotiwa na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon.

Vyanzo vya habari vimeiambia kanali hiyo inayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu kuwa, wanajeshi hao waliingia kambini hapo katika mji wa Shaddadi Jumatano iliyopita, wakiwa na lengo la kufanikisha njama za Marekani, Riyadh na waitifaki wao katika eneo za kuiba mafuta ya Syria.

Duru za habari zimedokeza kuwa, wanajeshi wapatao 20 wa Saudia wakiongozwa na kamanda anayefahamika kama Saud al-Joghaifi, walielekea Syria wakipewa ulinzi na msafara wa magari ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani, wakitokea katika kambi ya Taji, yapata kilomita 20 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Habari zaidi zinasema kuwa, kuwasili kwa askari hao wa Kisaudi nchini Syria kumesadifiana na kuwasili kwa malori 30 yenye mitambo ya kuchimba mafuta na watalaamu wa masuala ya uchimbaji mafuta wa Saudia na Misri wanaosadikiwa kuwa wafanyakazi wa shirika la Aramco la Aal-Saud.

Malori ya US yakibeba mafuta yaliyoibiwa Syria

Disemba mwaka jana pia, duru za habari zililiarifu shirika la habari la Anadolu la Uturuki kuwa, makumi ya wanajeshi wa Saudia wamewasili katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Omar katika mkoa wa mashariki wa Dayr al-Zawr, kwa ndege za helikopta.

Hii ni katika hali ambayo, nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki hivi karibuni zimetoa taarifa ya pamoja mwishoni mwa kikao cha tatu cha Kamati ya Katiba ya Syria zikilaani wizi wa mafuta unaofanywa na Marekani na waitifaki wake nchini Syria.

Tags

Maoni