Aug 30, 2020 11:10 UTC
  • Jeshi la Yemen lamtia mbaroni kamanda mwandamizi wa al-Qaeda

Vikosi vya Yemen vimetangaza habari ya kumtia nguvuni kamanda wa ngazi ya juu wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Kiarabu, Sana'a.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen, Brigedia Jenerali Abdul Khaleq al-Ajri amesema kamanda huyo mwandamizi wa al-Qaeda alitiwa mbaroni jana Jumamosi akitokea mkoa wa katikati mwa nchi wa Ma'rib.

Hata hivyo hakutaja jina wala uraia wa kamanda huyo wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ambao umeshaua maelfu ya watu katika hujuma zake hususan katika eneo la Asia Magharibi.

Al-Ajri amesema kamanda huyo ambaye alikuwa kinara wa magenge ya kigaidi katika eneo la Qaifa mkoani al-Bayda, alikuwa ameelekea Sana'a kwa lengo la kufanya operesheni za kigaidi mjini hapo.

Wanachama wa al-Qaeda nchini Yemen

Jumatano iliyopita, Kituo cha Habari za Usalama cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen kilitangaza kuwa, magenge ya kigaidi ya Daesh na al-Qaeda yamefanya mashambulizi 320 katika mkoa wa al-Bayda katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo jeshi la Yemen hivi karibuni lilitangaza kuwa limefanikiwa kukomboa kilomita mraba 1000 ya ardhi ya mkoa huo iliyokuwa mikononi mwa magenge ya kigaidi, sanjari na kuua magaidi 250 katika operesheni za kusafisha mabaki ya wanachama wa ISIS na al-Qaeda.

 

 

Tags