Sep 03, 2020 08:08 UTC
  • Arab League yawaacha mkono Wapalestina na kuunga mkono mapatano ya UAE na Wazayuni

Katika hatua inayoonyesha kuipiga vita na kuiacha mkono Palestina na badala yake kuunga mkono hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu ya kufanya mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imelikataa ombi la Palestina la kuitishwa kikao cha dharura cha jumuiya hiyo.

Kanali ya televisheni ya Al Mayadeen imeripoti kuwa Arab League imelikataa ombi la Palestina la kutaka kiitwishe kikao cha dharura cha jumuiya hiyo ili kutangaza upinzani dhidi ya hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel.

Imeelezwa kuwa ombi la Palestina limekataliwa kutokana na malalamiko ya Bahrain.

Baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimekuwa zikichukua hatua nyingine kuhusiana na kufikia maridhiano na utawala wa Kizayuni kwa kujaribu kuwa na ushawishi katika maamuzi ya Wapalestina na kuwashinikiza wakubali kujiunga na mpango wa kihaini wa 'Muamala wa Karne'.

Palestina ilikuwa imewasilisha pendekezo la kutaka kiongezwe kipengele cha kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Imarati na Israel katika kikao cha kawaida cha Arab League kilichopangwa kufanyika tarehe 9 Septemba.

Hata hivyo Bahrain imepinga ombi hilo na kuwatishia Wapalestina kuwa itawasilisha kipengele cha kuunga mkono kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na kushajiisha mpango wa Muamala wa Karne.

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani, tarehe 13 ya mwezi uliopita wa Agosti Imarati na utawala wa Kizayuni wa Israel zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Makubaliano hayo yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.../

Tags