Sep 06, 2020 02:26 UTC
  • Harakati ya PFLP yataka kutimuliwa Imarati katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina (PFLP) amesema kuwa, hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel inakinzana na uamuzi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu hivyo ametoa wito wa kutimuliwa nchi hiyo sambamba na kurejeshwa Syria katika jumuiya hiyo.

Abu Ahmad Fuad, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina (Popular Front for the Liberation of Palestine) amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya al-Masira na kueleza kwamba, uamuzi wa Imarati wa kuanzisha uhusiano na adui Mzayuni ni hatua ya hujuma dhidi ya wananchi wa Palestina na kwamba, watawala wa Abu Dhabi mbali na kuanzisha uhusiano huo na Israel wamekuwa na nafasi haribifu pia katika vita vya Yemen na kuharibiwa vibaya nchi hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina amesisitiza kuwa, uhusiano wa Imarati na Israel una mfungamano na uchaguzi wa Marekani na kuupa fursa na upendeleo utawala ghasibu wa Israel na kwamba, serikali ya Washington imekuwa ikiwatwisha Waarabu hususan Wapalestina hatua za kivamizi. 

Walimwengu wameendelea kulaani hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel wakisema ni usaliti na khiyana kwa Ulimwengu wa Kiislamu

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida kati ya Imarati na utawala haramu wa Kizayuni, tarehe 13 ya mwezi uliopita wa Agosti pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Hatua hiyo ya khiyana na usaliti uliofanywa na Imarati kwa Ulimwegu wa Kiislamu na malengo matukufu ya Wapalestina imeendelea kulaaniwa kila mahala.

Tags