Sep 09, 2020 13:36 UTC
  • Mtifuano wa ana kwa ana kati ya Palestina na asasi za Waarabu kuhusu Makubaliano ya Abraham

Kikao cha leo cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League kimefanyika wakati msimamo ulioonyeshwa na jumuiya hiyo pamoja na Baraza Kuu la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi GCC, hususan katika siku za karibuni kuhusu mapatano yaliyofikiwa kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni wa Israel umethibitisha kuwa, tajiriba ya uchukuaji maamuzi kitaasisi katika Ulimwengu wa Kiarabu imefeli;

na ukweli ni kwamba, taasisi za Waarabu hazina uwezo wa kutetea na kupigania maslahi ya wanachama wake ikiwemo Palestina.

Baada ya Imarati na utawala wa Kizayuni kuafikiana kuanzisha uhusiano wa kawaida kupitia mapatano ambayo ni maarufu kama Makubaliano ya Abraham (Abraham Accord), makundi ya Kipalestina pamoja na Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina zilichukua msimamo mmoja wa kulaani makubaliano hayo na kutilia mkazo pia ulazima wa kutumia mbinu ya muqawama wa mtutu wa bunduki. Msimamo huo wa pamoja ulionekana wazi zaidi kuliko wakati wowote ule katika kikao cha Alkhamisi iliyopita cha makatibu wakuu na maafisa wa makundi 14 ya Palestina kilichofanyika Beirut, mji mkuu wa Lebanon.

Si hayo tu, lakini Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina iliiomba Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iitishe kikao cha dharura kuhusiana na Makubaliano ya Abraham, lakini ombi hilo la Palestina lilikataliwa na jumuiya hiyo ambayo ilieleza kwamba suala hilo litajadiliwa katika kikao chake cha kawaida kitakachofanyika mwezi huu wa Septemba.

Kikao cha leo cha Arab League kimefanyika katika hali ambayo, msimamo dhaifu na legevu wa jumuiya hiyo kuu ya Waarabu kuhusiana na Makubaliano ya Abraham yamegeuka kuwa msimamo dhidi ya Palestina. Kuhusiana na hilo, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, Nayef Al Hajraf, ambaye taasisi hiyo iliyo chini ya uongozi wake hadi sasa si tu haijatoa kauli yoyote kuhusu makubaliano hayo, bali kwa namna fulani imeonyesha kuwa inayaunga mkono, siku ya Jumatatu alidai kwamba, baadhi ya washiriki wa kikao cha Beirut cha makundi ya Kipalestina walitoa kauli za vitisho na uchochezi; na kwa sababu ya jambo hilo Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inampasa aombe radhi.

Ijapokuwa shakhsia na makundi ya Wapalestina yametoa jibu kwa matamshi hayo ya Katibu Mkuu wa GCC, lakini kauli hiyo tu aliyotoa Al Hajraf, kwa upande mmoja imeonyesha kuwa kikao cha leo cha Arab League hakitatoka na msimamo mmoja wa kuitetea Palestina; na kwa upande mwingine Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina iko katika hali ya udhaifu na imelegeza msimamo kuhusiana na taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao cha Beirut, kuhusu muqawama wa mtutu wa bunduki.

Katibu Mkuu wa GCC, Nayef Al-Hajraf

Mwakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameelekea kwenye kikao cha leo cha Arab League akiwa amekusudia kuwasilisha rasimu ya azimio ambayo imehafifisha ukosoaji wa Palestina kwa nchi za Kiarabu na vilevile haitoi ombi lolote la kutaka Imarati ilaaniwe au ichukuliwe hatua kwa sababu ya kusaini Makubaliano ya Abraham na utawala haramu wa Israel. Lakini kabla ya hapo, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilikuwa imetamka bayana kuwa, mapatano ya Imarati na utawala wa Kizayuni ni usaliti na sawa na kulichoma jambia la mgongo taifa la Palestina.

Kuna nukta kadhaa za kuashiriwa hapa kuhusu misimamo iliyoonyeshwa na jumuiya za Kiarabu pamoja na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa Makubaliano ya Abraham.

Nukta ya kwanza ni kwamba, mshindwa mkuu wa makubaliano ya Abraham ni Mamlaka ya Ndani ya Palestina, kwa sababu makubaliano hayo yameonyesha kuwa, muelekeo inaofuata mamlaka hiyo wa kutumia mbinu ya kufanya mazungumzo, mapatano na ushirikiano wa kiusalama na utawala wa Kizayuni, kiuhalisia umefeli. Nukta hiyo ilitiliwa mkazo pia katika kikao cha Alkhamisi iliyopita kilichofanyika Beirut. Matunda na matokeo ya mtazamo wa kufanya mapatano uliyonayo Mamlaka ya Ndani ya Palestina yamekuwa ni makubaliano yaliyofikiwa kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni, ambayo Netanyahu ameyapa jina la “Amani Mkabala na Amani”, ikiwa na maana kwamba, si tu hakutakuwa na sehemu yoyote ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu itakayorejeshwa kwa Wapalestina, lakini utawala wa Kizayuni utatekeleza pia azma yake ya kupora asilimia 30 ya eneo la Ufukwe wa Magharibi.  

Nukta nyingine ya pili ni kwamba, Makubaliano ya Abraham yamelenga waziwazi moja ya masuala muhimu zaidi ya Ulimwengu wa Kiarabu, yaani Palestina; lakini msimamo uliochukuliwa na jumuiya za Waarabu, hususan Arab League na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kuhusiana na makubaliano hayo umeonyesha kuwa, jumuiya hizo si watetezi wa maslahi ya nchi wanachama, bali ni nyenzo tu zinazoitumikia Saudi Arabia na waitifaki wake ikiwemo Imarati na Bahrain, lakini zenyewe, hazina uwezo kiutendaji wa kutetea na kupigania maslahi ya nchi wanachama. Na ndiyo kusema kuwa, Makubaliano ya Abrahman yamethibitisha rasmi kufeli kwa tajiriba ya kitaasisi katika Ulimwengu wa Kiarabu…/

 

Tags