Sep 10, 2020 10:56 UTC
  • Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na udhaifu katika kutetea maslahi ya Waarabu

Kikao cha Jumatano ya jana cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Kiarabu (Arab League) kilichofanyika kwa njia ya video, kilimaliza kazi zake kwa kuunga mkono mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Imarati na Israel.

Kikao hicho cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kimefanyika yapata mwezi mmoja tu baada ya kutangazwa mapatano ya kuanzisha uhusiano baina ya pande hizo mbili. Mwishoni mwa kikao hicho hakukutolewa taarifa yoyote ya kulaani hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala unaoendelea kuua raia wa Palestina, na zaidi ni kwamba, kimeyaunga mkono mapatano hayo kwa njia moja au nyingine. 

Swali muhimu linalojitokeza hapa ni kwamba, ni kwa nini Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inashindwa kutetea maslahi ya nchi wanachama?

Kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Inaonekana kuwa, sababu ya udhaifu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni "kutokuwepo msimamo wa pamoja" ndani ya jumuiya hiyo kwa ajili ya kutetea maslahi ya nchi za Kiarabu. Katika jumuiya hiyo ya nchi za Kiarabu hakuna mwafaka kuhusiana na jinsi ya kuamiliana na makubaliano ya Imarati na Israel ambayo yamekuwa maarufu kwa jina la "Mkataba wa Abraham" (Abraham Accord). Baadhi ya nchi za Kiarabu kama Misri, Oman, Bahrain na Mauritania zimeyaunga mkono rasmi huku nchi kama Saudi Arabia, Qatar na Jordan zikitoa ishara ya kuyakubali, na nchi nyingine zikikhitari kunyamaza kimya au kuyapinga. 

Sababu nyingine ni kwamba nchi wanachama katika Arab League hazina uzito sawa ndani ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Jumuiya hiyo inadhibitiwa na baadhi tu ya nchi za Kiarabu ambazo haziko huru wala hazijitegemei katika kuchukua maamuzi yanayohusiana na siasa za kigeni, na haziwezi kuchukua harakati ya aina yoyote katika eneo la magharibi mwa Asia nje ya sera na siasa za Marekani. Ni kwa msingi huo ndiyo maana tunaona kuwa, baada ya Marekani kubuni na kusimamia mapatano ya Imarati na utawala haramu wa Israel, hakuna uwezekano wa nchi za Kiarabu kusimama na kupinga au hata kuulaani kwa maneno mapatano hayo.

Tramp na watawala vibaraka wa Marekani

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa miongoni mwa athari za Mkataba wa Abraham ni kuongezeka ushawishi wa Marekani na utawala haramu wa Israel katika ulimwengu wa Kiarabu. Dawood Shihab ambaye ni msemaji wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina (PIJ) anasema: "Jumuiya ya Nchi za Kiarabu sasa imekuwa kinara mkuu wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi za jumuiya hiyo na utawala haramu wa Israel na inatupilia mbali nafasi yake asili kwa maslahi ya kuzidisha satua na ushawishi wa Marekani na utawala wa Kizayuni."

Sababu ya tatu ya udhaifu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni kwamba licha ya kuwa jumuiya hiyo ilianzishwa kwa msingi wa utaifa na kaumu ya Waarabu lakini inaonekana kuwa, sasa inatupilia mbali suala hilo wakati wa kuchukua maamuzi muhimu yanayohusiana na siasa za nje. Imarati, Bahrain, Misri, Jordan na Saudi Arabia kwa kiasi fulani ni miongoni mwa nchi za Kiarabu zinazofuata sera hiyo ya kutupilia mbali utaifa wa Kiarabu katika kupanga siasa zao za nje. Ni kwa msingi huo ndiyo maana suala la Palestina halikujadiliwa kwa undani katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Kirabu na badala yake, Bahrain na Imarati zimeituhumu Palestina kuwa inataka kuzusha hitilafu na mgawanyiko katika jumuiya hiyo!

Donald Trump akiwa pamoja na Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdul Aziz

Sababu ya nne iliyoifanya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ishindwe kulinda maslahi ya nchi za Waarabu ni kwamba sasa jumuiya hiyo inajitambua kuwa wajibu wake ni "kuwalinda watawala wa Kiarabu na si mataifa ya Kiarabu". Wananchi katika aghlabu ya nchi za Kiarabu wamepinga mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Imarati na Israel na wamechoma moto bendera za Umoja wa Falme za Kiarabu na picha za mrithi wa utawala wa nchi hiyo; lakini kambi ya wafalme na watawala wa Kiarabu wenye madaraka wamesimama na kukabilia na upinzani huo wa wananchi. Kwa msingi huo msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) Hazim Qassem amekosoa kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu cha Jumatano ya jana na kusema: "Misimamo ya jumuiya hiyo haiakisi upinzani wa mataifa ya Kiarabu dhidi ya suala la kuanzishwa uhusiano baina ya nchi hizo na utawala haramu wa Israel."     

Tags