Sep 11, 2020 04:45 UTC
  • Ismail Haniya: Kutolaani kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel ni kuhudumia maslahi ya Wazayuni

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, kupingwa muswada wa Palestina kuhusu kulaaniwa uanzishaji uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni kuhudumia maslahi ya utawala huo ghasibu.

Ismail Haniya ameashiria hatua ya jana ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ya kutolaani mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel na kuonya kuhusiana na hatua hiyo.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS  amebainisha kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel ni kuushambulia wazi Umma wa Kiislamu na haki zao.

Haniya amesisitiza kuwa, Palestina ni kadhia ya Umma wa Kiislamu na Quds ni suala linalounganisha Umma wa Kiislamu na Kiarabu.

 

Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu walipokutana katika kikao chao Machi 2019

Jana Jumatano, baadhi ya nchi za Kiarabu zilipinga muswada uliowasilishwa na Palestina katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa kutaka kulaaniwa hatua ya Imarati ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani ili kurahisisha mchakato wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel, tarehe 13 Agosti Umoja wa Falme za Kiarabu UAE na Israel zilitangaza kuwa zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baina yao.

Makubaliano hayo yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.

Tags

Maoni