Sep 12, 2020 11:27 UTC
  • Jordan: Ufunguo wa amani Asia Magharibi ni kutoghusubiwa ardhi za Wapalestina

Jordan imesema njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Palestina na kupatikana amani ya kudumu katika eneo la Asia Magharibi ni kukomesha mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel wa kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Ayman Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan amesema hayo muda mfupi baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa Bahrain na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.

Safadi ameeleza bayana kuwa: Kuundwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu na kwa kujibu wa Mipaka ya Mwaka 1967, inasalia kuwa ufunguo wa amani na kutamatisha mgogoro katika eneo, kama unavyoashiria Mpango wa Amani wa Waarabu na maazimio ya kimataifa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jordan ameonya kuwa, hatua yoyote ya kuvuruga fursa za kupatikana amani ya kudumu katika eneo na kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu hakutakuwa na matokeo mengine isipokuwa kushadidisha mgogoro uliopo.

Wajordan katika maandamano ya kuunga mkono kadhia ya Palestina

Julai mwaka huu, maelfu ya wananchi wa Jordan waliandamana na kutangaza upinzani wao dhidi ya mpango wa utawala haramu wa Israel wa kutaka kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina.

Aidha Mfalme Abdallah II wa Jordan naye sambamba na kutangaza kuunga mkono maslahi ya wananchi wa Palestina alisema bayana kwamba, serikali ya nchi hiyo inapinga hatua yoyote ile ya upande mmoja ya Israel ya kutwaa ardhi ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina.

Tags

Maoni