Sep 14, 2020 06:33 UTC
  • Sayyid Hakim: Kamwe Iraq haiwezi kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel

Kiongozi wa mrengo wa kitaifa wa al-Hikma nchini Iraq amesema katu taifa hilo la Kiarabu haliwezi kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Sayyid Ammar al-Hakim alisema hayo jana Jumapili katika mkutano wake na kundi la wasomi na wanafikra na kueleza bayana kuwa, ajenda ya kuundwa taifa huru la Palestina itaendelea kubakia hai.

Mwanaharakati na msomi huyo mashuhuri wa Kiislamu nchini Iraq ameitaja hatua ya Imarati na Bahrain ya kuutambua rasmi utawala wa Kizayuni wa Israel na kutangaza kuwa tayari kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu kuwa ni kosa la kistratejia. 

Maandamano ya kulaani kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel yameshuhudiwa katika maeneo mbalimbali duniani

Sayyid Hakim ambaye pia ni mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq amesisitizia udharura wa kuwepo utangamano wa kitaifa baina ya Baghdad na Arbil, sanjari na kubuniwa mpango wa kuyaleta pamoja makundi yote ya Iraq. Amesema mkakati huo utapelekea kuwepo uthabiti wa kisiasa katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Akthari ya mataifa ya Kiislamu ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamelaani vikali uamuzi huo wa kifidhuli wa UAE na Bahrain wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Israel, yakisisitiza kuwa, kitendo hicho hakitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuzidisha taharuki katika eneo la Asia Magharibi.

Tags

Maoni