Sep 17, 2020 05:57 UTC
  • Mapatano ya kuanzisha uhusiano na Israel ni dhambi isiyosameheka

Nchi za Imarati na Bahran juzi Septemba 15 zilisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Sherehe ya kutiwa saini mapatano hayo ilifanyika ikulu ya White House mjini Washington chini ya usimamizi wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati Abdallah bin Zayed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain Abdullatif al Zayani, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Donald Trump wamedai kuwa mapatano hayo yanaandaa uwanja wa kuhitimishwa mapigano na kupatikana amani katika eneo la Asia Magharibi. Madai hayo yametolewa katika hali ambayo agahalabu ya wachambuzi huru wa mambo wanaamini kuwa, mapatano hayo ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili za Kiarabu na Israel si tu hayatasaidia kupatikana amani katika eneo la Mashariki ya Kati bali ni pia "dhambi isiyosameheka."

Kuna sababu nyingi zinazothibitisha na kutia mguvu mtazamo huu wa wataalamu wa mambo..

Ya kwanza na yenye umuhimu zaidi ni kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel si tu haijaachia sehemu yoyote ya ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina mkabala na kufikiwa mapatano hayo bali pia haujasitisha uvamizi na kuyakalia kwa maeneo zaidi ya Palestina. Wakati huo huo, utawala wa Kizayuni unaendeleza mzingiro wake wa kidhulma wa miaka 14 dhidi ya eneo la Ukanda wa Ghaza.  

Katika mazingira kama hayo, hatua ya Imarati na Bahrain ya kufikia mapatano na Israel ni kuunga mkono kivitendo uvamizi na jinai zinazofanywa utawala wa Kizayuni na kuzidisha uhalifu huo

Netanyahu, Bin Zayed na al Zayani wakiwa White House 

David Yaaqubian ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu nchini Marekani amezungumzia suala hilo akisema: "Watawala wa Imarati na Bahrain badala ya kutafuta amani na usalama miongoni mwa wananchi na kushirikiana na nchi za knda ya Mashariki ya Kati, wameelekeza mtazamo wao liojaa njozi kwa Netanyahu na Donald Trump. Hii ndio maana mapatano hayo ya kuanzisha uhusiano baina ya tawala hizo na Israel yakatajwa kuwa na dhambi isiyoweza kusameheka.

Sababu ya pili ni kuwa, mapatano hayo ya kuanzisha uhusiano kivitendo yamekwenda sambamba na kudhalilishwa Imarati na Bahrain. Utawala wa Kizayuni wa Israel hivi sasa unakabiliwa na changamoto chungu nzima za ndani katika nyanja za kisiasa, kiusalama na kiuchumi. Hatua ya utawala wa Kizayuni ya kufanya mapatano na Imarati na Bahrain inaweza kudhamini fursa za kiusalama na kiuchumi kwa utawala huo. Hata hivyo Donald Trump amedai katika hafla ya kutiwa saini mapatano hayo kuwa yatapelekea kupatikana fursa zaidi za kiuchumi na kimaendeleo kwa ajili ya nchi hizo mbili.

Kwa maneno mengine ni kuwa Rais wa Marekani anaamini kwamba, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain zilikuwa zikiyahitajia zaidi mapatano hayo kuliko utawala wa Kizayuni.

Imarati na Bahrain pia hazikupata lolote huko Marekani ghairi ya kudhalilishwa na kudunishwa ujumbe wa nchi hizo mbili uliokwenda Washington kutia saini mapatano hayo. Kwa mfano tu Abdullatif al Zayani Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain alilakiwa na ujumbe wa ngazi ya chini na kuachwa kwenye mataa na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Marekani. Mienendo ya aina hii pamoja na hatua ya Trump kuzitambua nchi hizo kuwa ni "ng'ombe wa kukamuliwa maziwa" kutokana na fedha zao za mapato ya mafuta, ni kielelezo cha jinsi Rais wa Marekani anavyozidunisha na kuzidhalilisha nchi hizo za Kiarabu. 

Rais Donald Trump wa Marekani  

Sababu nyingine ambayo inayafanya mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baina ya nchi hizo za Kiarabu na utawala katili wa Israel kuwa dhambi isiyosameheka ni kuwa, mapatano hayo yamesababisha ufa na migawanyiko zaidi. Sehemu kubwa ya mataifa na nchi za Kiislamu zimepinga mapatano hayo na kutayaja kuwa ni usaliti kwa Palestina na kwa Ulimwengu wa Kiislamu. Baadhi ya nchi pia zimeunga mkono wazi mapatano hayo waziwazi au kwa njia isiyo ya moja ka moja. Hali hiyo inaonyesha kuwa mapatano ya kuanzishwa uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel yameibua migawanyiko ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu na dhambi hii haisameheki. 

Tags

Maoni