Sep 17, 2020 08:11 UTC

Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema muqawama ni chaguo la Wapalestina wote dhidi ya utawala wa Kizayuni, na kwamba makundi ya mapambano hayana mistari myekundu katika vita dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Ziyad al-Nakhalah alisema hayo jana Jumatano katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon na kuongeza kwamba, "hakuna mistari myekundu katika harakati za muqawama dhidi ya mvamizi. Israel nzima ni shabaha ya wanamuqawama iwapo vita vitaibuka."

Amebainisha kuwa, vikosi vya muqawama vimesimama kidete na vipo tayari kabisa katika vita tarajiwa na Israel na kwamba maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo pandikizi yatakuwa shabaha ya makombora ya wanamuqawama.

Sambamba na kuwataka viongozi wa Palestina kubuni muungano wa pamoja wa kisiasa mkabala wa utawala ghasibu wa Israel, Katibu Mkuu wa Jihadul Islami amesisitiza kuwa: Karibuni tutapiga mahesabu mapya yatakayopelekea kuchukuliwa hatua za pamoja za kijeshi. Tumefungamana na Palestina kuanzia baharini hadi mitoni na hii ni haki yetu.

Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina

Baada ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Kizayuni unaokikalia kwa mabavu Kibla cha Kwanza cha Waislamu, juzi Jumanne, Imarati na Bahrain zilikwenda kutia saini makubaliano hayo mbele ya Donald Trump na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huko Washington, Marekani.

Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ameongeza kuwa, kitendo cha ndege za Israel kuruka juu ya miji mitakatifu ya Makka na Madina ni idhilali, ambapo pia amezishukuru Iran na Uturuki kwa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

Tags

Maoni