Sep 18, 2020 08:10 UTC
  • Tofauti baina ya Mapatano ya Abraham, Camp David na Wadi Araba

Nchi za Kiarabu zimesaini mapatano mara tatu na utawala wa Kizayuni wa Israel na ya hivi karibuni zaidi kati ya mapatano hayo ni yale yliyopewa jina la Mapatano ya Abraham (Abraham Accords) yaliyosainiwa tarehe 15 mwezi huu wa Septemba katika Ikulu ya Rais wa Marekani, White House. Mapatano hayo matatu yana tofauti kadhaa na muhimu.

Tarehe 15 mwezi huu wa Septemba nchi za Imarati na Bahrain zilitia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel. Mapatano hayo ya Abraham ni ya tatu baina ya nchi za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel. Mbali na mapatano ya Abraham, Camp David na Wadi Araba kuna Mapatano ya Oslo ambayo hata hivyo yalitiwa saini na Wapalestina na utawala huo katili na si baina ya Israel na nchi nyingine ya tatu. 

Mfanano uliopo katika mapatano hayo matatu ni kwamba Marekani imekuwa na nafasi kubwa sana katika kufikiwa kwake. Vilevile mapatano hayo yote yamesainiwa katika kipindi cha nusu ya pili ya mwaka. Mapatano ya Camp David yalitiwa saini tarehe 17 Septemba 1978 baina ya Misri na utawala haramu wa Israel, yale ya Abraham yametiwa saini mwezi huu wa Septemba, na Mapatano ya Wadi Araba yalifanyika tarehe 26 Oktoba mwaka 1994 baina ya Israel na Jordan. 

Pamoja na hayo kuna tofauti kubwa na muhimu baina ya mapatano hayo. Kwanza ni kuwa, Mapatano ya Camp David yalitiwa saini baada ya vita vya nchi za Misri na Jordan na utawala wa Kizayuni wa Israel, na katika vita vyote vinne vya mwaka 1948, 1956, 1967 na 1973 Misri na Jordan zilishindwa mkabala wa Israel. Hii ni katika hali ambayo Imarati na Bahrain hazikuwa na vita na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kinyume chake, zimekuwa na uhusiano wa siri na utawala huo. 

White House

Tofauti ya pili ni kwamba, Misri na Jordan zilisaini mapatano ya Camp David na Wadi na Araba na utawala wa Kizayuni wakati zina mpaka wa pamoja na utawala huo ghasibu na zilikuwa na hitilafu za mpaka na utawala huo. Hali hii ni tofauti na Bahrain na Imarati ambazo hazina mpaka wa pamoja na utawala huo haramu na ziko mbali kabisa kijiografia na mipaka ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Tofauti ya tatu ni kwamba, katika Mpatano ya Camp David na Wadi Araba sehemu ya ardhi iliyokuwa ikikaliwa kwa mabavu na Israel ilirejeshwa. Katika mapatano ya Camp David, Misri ilirejeshewa eneo la jangwa la Sinai lililokaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya siku sita baina ya pande hizo mbili mkabala wa kuutambua rasmi utawala huo. 

Katika Mapatano ya Wadi Araba, Jordan iliyakodisha kwa kipindi cha miaka 25 maeneo mawili ya al Baqura na al Ghamr ambayo yalikuwa yakikaliwa kwa mabavu na utawala huo na ikawa imeyakomboa kwa njia moja au nyingine. Novemba mwaka 2019 muda wa kukodishwa maeneo hayo kwa Israel ulimalizika na serikali ya Jordan ikatangaza rasmi kuhitimishwa kipindi hicho. Ama katika mapatano ya Bahrain na Imarati na utawala wa Kizayuni hakuna ardhi yoyote iliyokombolewa, na madai yaliyotolewa na Abu Dhabi katika uwanja huo yalikuwa uongo ambao umekadhibishwa hata na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. 

Donald Trump na Netanyahu

Tofauti ya nne ni kuwa Mapatano ya Camp David na Wadi Araba yalitiwa saini katika zama za marais wawili kutoka chama cha Democratic. Camp David ilisainiwa katika utawala wa Jimmy Carter na Wadi Araba ilisainiwa katika kipindi cha Bill Clinton, na marais hao wawili walikuwa Wademokrati na walikuwa wakiunga mkono suala la kuundwa dola la Palestina. Mapatano ya Abraham yamesainiwa chini ya utawala wa Donald Trump, Mripublican ambaye mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020 alizindua mpango wa Muamala wa Karne ambao ni dhidi ya Wapalestina na haukubaliani na suala la kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds Mashariki. Mpango huo habithi unautambua mji wote wa Quds tukufu kuwa ni mali ya utawala haramu wa Israel. 
Tofauti hizo zinaonesha kuwa, Mapatano ya Abraham hayana matunda ya aina yoyote kwa tawala za Imarati na Bahrain na mshindi katika mapatano hayo ni utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Tags

Maoni