Sep 18, 2020 10:34 UTC
  • Sababu za kutoundwa serikali ya Waziri Mkuu wa Lebanon Mustapha Adib

Licha ya kupita majuma mawili tangu Mustapha Adib, Waziri Mkuu wa Lebanon akabidhiwe jukumu la kuunda serikali, lakini hadi sasa bado hajafanikiwa kutekeleza hilo.

Kuanzia tarehe 4 ya mwezi uliopita wa Agosti, Lebanon imeshuhudia matukio makubwa. Katika siku hiyo, mlipuko mkubwa ulitokea katika bandari ya Beirut na kusababisha zaidi ya watu 170 kuuawa na wengine takribani 7,000 kujeruhiwa. Baada ya mlipuko huo, kuliibuka malalamiko na maandamano ya wananchi ambapo baadhi yao walikuwa wakiungwa mkono ndani ya Lebanon huku waandamanaji wengine wakipata himaya na uungaji mkono kutoka nje. Waandamanaji hao walifanikiwa kudhibiti majengo ya wizara kadhaa.

Kufuatia hali hiyo, tarehe 10 ya mwezi huo huo yaani Agosti iliyopita, aliyekuwa Waziri Mkuu Hassan Diab akatangaza kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu Hassan Diaba, tarehe 13 mwezi uliopita, Bunge la Lebanon lilipitisha kwa wingi wa kura jina la Mustapha Adib aliyekuwa amependekezwa na Rais Michel Aoun kushika wadhifa wa Waziri Mkuu.

Hassan Diab, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyejiuzulu

 

Sanjari na kuchaguliwa Waziri Mkuu wa Lebanon, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alifanya safari nchini Lebanon ikiwa ni safari yake ya pili nchini humo katika kipindi cha mwezi mmoja. Awali Macron alifanya safari nchini Lebanon Agosti 6 yaani siku mbili tu baada ya mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut. Katika safari yake ya pili katika nchi hiyo ya Kiarabu, Rais wa Ufaransa alitangaza kuwa, serikali mpya ya nchi hiyo inapaswa kuundwa katika kipindi cha siku 15. Pamoja na hayo na licha ya kupita siku 17, lakini hadi sasa Mustapha Adib  hajafanikiwa kuunda serikali.

Mustapha Adib amekumbwa na mkwamo katika kuunda serikali katika hali ambayo, shakhsia huyo aliungwa mkono na mirengo ya ndani na ya nje wakati alipokabidhiwa wadhifa wa Waziri Mkuu. Kwa muktadha huo, swali la kimsingi kwa sasa ni kwa nini Mustapha Adib hadi sasa ameshindwa kuunda baraza jipya la mawaziri ilihali anaungwa mkono na pande zote za ndani na za nje?

Sababu ya kwanza inahusiana na mfumo wa kisiasa wenye mielekeo ya kimakundi nchini Lebanon. Mashia, Masuni na Wakristo wanagawana madaraka sawa bin sawia nchini humo. Mfumo huu hauna uratibu wowote baina ya kundi hili na kundi jengine. Pande tatu zinazounda madaraka nchini Lebanon yaani Mashia, Masuni na Wakristo kila mmoja kati ya makundi haya linafuatilia hisa yake. Kimsingi ni kuwa, moja ya sababu kuu za kusambaratika haraka serikali ya Hassan Diab inahusiana na muundo huu wa kikaumu nchini Lebanon.

Rais Michel Apun wa Lebanon

 

Filihali pia, katika mchakato wa kuunda serikali, baadhi ya mirengo yenye mielekeo ya Umagharibi inafanya juhudi za kudhibiti wizara muhimu ili kwa njia hiyo zipunguze uzito wa muungano wa muqawama katika muundo wa madarakani nchini humo.

Katika uwanja huo, mrengo wa al-Wafaa Lil-Muqawamah unaofungamana na Harakati ya Muqawama ya Hizbullah katika Bunge la Lebanon umetangaza kuwa, baadhi ya shakhsia ndani ya Lebanon inamzuia Waziri Mkuu aliyepewa jukumu la kuunda serikali kufanya mazungumzo na mirengo mbalimbali.

Sababu ya pili ya kuchelewa kuundwa serikali ya Waziri Mkuu Mustapha Adib nchini Lebanon inahusiana na uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu. Licha ya kuwa, Ufaransa imetangaza kuwa, inataka kuundwa haraka serikali ya Lebanon, lakini imekuwa ikiingilia rasmi na wazi kabisa mwenendo wa uarifishwaji majina ya mawaziri hususan wizara muhimu.

Baadhi ya duru za Lebanon zimetangaza kuwa, Ufaransa inafanya njama za kuzuia Wizara ya Hazina isichukuliwe na Harakati ya Amal au Harakati ya Hizbullah, jambo ambalo limekabiliwa na radiamali ya Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon. Berri ametangaza bayana kwamba, endapo chaguo la Waziri wa Hazina halitakuwa miongoni mwa Harakati ya Amal au Hizbullah, pande hizo mbili hazitashiriki katika uundaji wa serikali.

Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon

 

Nukta yenye umuhimu ni kwamba, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon inaamini kuwa, Ufaransa inaingilia mchakato wa uundwaji wa serikali ya Lebanon kwa amri ya Marekani. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana mrengo wa al-Wafaa Lil-Muqawamah katika Bunge la Lebanon, umeionyoshea kidole cha lawama serikali ya Marekani na kusema wazi kuwa, inafanya njama za kuvuruga juhudi za kuundwa serikali mpya nchini humo.

Kuchelewa kuundwa serikali ya Waziri Mkuu Mustapha Adib kunashuhudiwa katika hali ambayo, mlipuko wa bandari ya Beirut kwa akali umeisababishia nchi hiyo hasara ya dola bilioni 15 za Kimarekani; hivyo basi kuna udharura wa kuharakishwa mwenendo wa uundaji serikali hiyo na serikali ya muda ikabidhi majukumu yake kwa serikali yenye haki ya kuchukua maamuzi.

Maoni