Sep 18, 2020 10:39 UTC
  • Bunge la Ulaya
    Bunge la Ulaya

Bunge la Ulaya limetaka utawala wa Saudi Arabia uwekewe vikwazo vya silaha kutokana na kuhusika na mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa zamani wa utawala huo, Jamal Khashoggi na vilevile kwa kuua raia wasio na hatia katika vita vya Yemen.

Katika ripoti yake kuhusu mauzo ya silaha iliyopasishwa jana Alkhamisi, Bunge la Ulaya limezitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya kupinga mauaji yaliyofanywa na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya Jamal Khashoggi kwa kufuata kigezo cha nchi za Ujerumani, Finland na Denmark na kubana mauzo ya silaha kwa utawala wa Riyadh.

Jamal Khashoggi mwandishi habari aliyekuwa akiishi Marekani na mkosoaji wa Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia aliuawa kikatili na maajenti wa serikali ya Riyadh Oktoba Pili mwaka 2018 ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia huko Istanbul nchini Uturuki. 

CIA: Khashoggi aliuawa kwa amri ya mrthi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman

Baada ya kupitia siku 18 za kukaa kimya na kukana kuhusika kwake na jinai hiyo, hatimaye serikali ya Saudia na kutokana na mashinikizo ya kimataifa, ililazimika kukiri kwamba mwandishi huyo aliuawa ndani ya ubalozi wake mjini Istanbul. Taarifa za kiintelijensia ikiwemo ripoti ya shirika la ujasusil Marekani CIA zilionyesha kwamba Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia ndiye muhusika mkuu wa mauaji hayo ya kinyama. 

Ripoti iliyopasishwa jana na Bunge la Ulaya pia imesema kuwa, silaha zilizouzwa kwa Saudi Arabia, Imarati na nchi nyingine washirika wa Riyadh zimetumika kuua raia nchini Yemen ambako watu milioni 22 wanahitajia misaada ya kibinadamu.

Mashirika na jumuiya za kimataifa zimekuwa zikiilaumu Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kushirikiana na Saudi Arabia katika mauaji ya kikatili dhidi ya taifa la Yemen.  

Maoni