Sep 20, 2020 02:38 UTC
  • Wall Street Journal: Mfalme Salman ametofautiana na mrithi wake kuhusu kuanzisha uhusiano na Israel

Gazeti la Wall Street Journal la Marekani limefichua kuwa, kumetokea hitilafu kubwa na kali baina ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudi Arabia na mrithi wake, Muhammad bin Salman baada ya mapatano ya Imarati na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili.

Gazeti hilo limefichua kuwa mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman alitaka kusaini mapatano na kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel baada ya Imarati na Bahrain, lakini Mfalme Salman amepinga uamuzi huo.

Wall Street Journal  limeandika kuwa, kwa miaka mingi Mfalme Salman amekuwa akitaka kususiwa Israel na kuundwa nchi huru ya Palestina lakini mwanaye, Muhammad bin Salman, anataka kuanzisha uhusiano wa kibiashara na Israel na kuundwa kambi moja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutupiliwa mbali fikra kwamba, mgogoro wa Wapalestina na Israel ndiyo kadhia nambari moja ya ulimwengu wa Kiarabu.

Gazeti hilo limefichua kwamba Mfalme wa Saudia alishtushwa sana na tangazo la Rais Donald Trump wa Marekani hapo tarehe 13 mwezi Agosti kuhusu mapatano ya kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Imarati na utawala haramu wa Israel na kwamba sababu ya mshtuko huo ni kwamba Bin Salman hakumjulisha mapema baba yake kuhusu mapatano hayo.

Wall Street Journal limeandika kuwa, baada ya upinzani huo wa Mfalme Salman, mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Bin Salman alimjulisha mshauri mkuu wa Donald Trump, Jared Kushner kwamba baba yake hakubaliani na suala la kuanzishwa uhusiano wa waziwazi na Israel katika kipindi cha sasa.

Bin Salman alisema suala pelee linaloweza kufanywa na Saudi Arabia kwa sasa ni kuishawishi nchi ndogo ya Bahrain kufanya mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.

Nchi za Imarati na Bahran Septemba 15 zilisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Sherehe ya kutiwa saini mapatano hayo ilifanyika ikulu ya White House mjini Washington chini ya usimamizi wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Makubaliano hayo ya kusaliti malengo matukufu ya Palestina yamelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Tags

Maoni