Sep 20, 2020 02:39 UTC
  • Ansarullah: Kuanzisha uhusiano na Israel ni kuhudumia kampeni za uchaguzi wa rais za Trump

Harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imetangaza kuwa hatua ya nchi za Imarati na Bahrain ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel ni kumhudumia Donald Trump katika kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani.

Msemaji wa harakati ya Ansarullah, Mohammed Abdul-Salam amesema kuwa, lengo la baadhi ya nchi kutangulia mbele na kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kutaka kuzifungulia njia nchi nyingine katika mkondo huo na kuhalalisha kitendo hicho kiovu ili nchi zinazopinga suala la kuanzishwa uhusiano na utawala ghasibu wa Israel zijiunge na mwenendo huo.

Mohammed Abdul-Salam amesema kuwa, iwapo mwenendo wa kuanzisha uhusiano na utawala katili wa Israel utakamilika, kadhia ya Palestina itatupiliwa mbali, na Wazayuni watakuwa na uhuru wa kufanya lolote katika eneo hili la magharibi mwa Asia.

Mohammed Abdul-Salam

Msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, katika hatua ya kwanza kabisa taifa la Palestina linapaswa kusimama na kupinga mwenendo huo, na harakati za mapambano na tawala za nchi mbalimbali zinapaswa kuwasaidia Wapalestina na kuheshimu malengo na mapambano yao. 

Abdul-Salam amesema kuwa, ni ndoto na sarabi tupu kutegemea misimamo rasmi ya nchi za Kiarabu katika kadhia ya Palestina.  

Tags

Maoni