Sep 20, 2020 08:01 UTC
  • Yaliyomo kwenye mpango wa Marekani wa kutaka kumuengua Mahmoud Abbas

David Friedman, Balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) Alhamisi iliyopita alisema kuwa; Marekani inafikiria kumweka Mohammed Dahlan, kiongozi wa zamani wa harakati ya Fat-h kwenye uongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuchukua nafasi ya Mahmoud Abbas, rais wa sasa wa mamlaka hiyo.

Hapa kuna nukta kadhaa muhimu kuhusiana na matamshi hayo ya David Friedman. 

Ya kwanza ni kuwa, uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi nyingine ni kati ya stratejia yenye umuhimu mkubwa zaidi katika siasa za nje za Marekani.  Marekani yenyewe inajidai kuwa ni kiongozi wa dunia; na inajigamba kuhusu suala hilo na kutishia hata kuziondoa madarakani serikali zinazokataa kufuata sera zake. Kadhia hii ilitokea mwaka 2019 huko Iraq. Adel Abdulmahdi Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq ambaye alikuwa akipigania kujitawala na kujichukulia maamuzi yake yenyewe nchi hiyo kuhusiana na siasa za nje alikabiliwa na hasira za Marekani. Mwezi Oktoba mwaka 2019 Marekani ilipanga maandamano dhidi ya serikali ya Iraq yaliyofanywa na  vibaraka wake na kumuandalia mazingira Adel Abdulmahdi ya kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Sababu iliyoifanya Marekani imkasirikie Abdulmahdi ni mapatano yaliyofikiwa kati ya Iraq na China kwa kwa ajili ya kushirikiana kistratejia na pia kukataa Abdulmahdi kuunga mkono vikwazo  vya Marekani dhidi ya Iran. 

Adel Abdulmahdi,  Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq  

Nukta ya pili ni kuwa, Marekani haiamini kanuni ya kistratejia ya haki ya kujitawala. Ukweli ni kuwa viongozi wa Marekani wanaikubali kanuni hii kwa viongozi na nchi zinazounga mkono sera zake tu. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuhusu suala hilo kwamba moja ya sababu iliyopelekea kufikiwa mapatano kati ya Imarati na Bahrain na utawala wa Kizayuni ni mashinikizo mengi ya White House kwa watawala wa nchi hizo. Kusalia madarakani kwa Mohammed bin Zayed mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi na Mfalme wa Bahrain Sheikh Hamad bin Issa Aal Khalifa kunategemea uungaji mkono wa Marekani. Moja ya ishara za kutoamini uhakika wa mambo Marekani kuhusu kanuni hiyo ya haki ya kujiainishia mustakbali ilikuwa ni uingiliaji wake katika mapambano ya ukombozi ya nchi za Kiarabu ya mwaka 2011 na kupotosha mapambano hayo. Jitihada za kutaka kumuengua madarakani Mahmoud Abbas pia zinaweza kutathminiwa katika uwanja huo; hatua ambayo imekabiliwa na radiamali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina.  Mohammad Shtayyeh Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amejibu matamshi ya David Friedman kwa kusema:  Marekani ipo njozini; iwapo inadhani kama inaweza kuwatwisha wananchi wa Palestina irada na matakwa yake.  

Nukta ya tatu ni kuwa, Marekani imeweka muda wenye mpaka maalumu wa kuwatumia shakhsia mbalimbali duniani; na watu hao wataungwa mkono na Marekani madhali wataendelea kutii siasa za Washington. Marekani itachukua hatua ya kuwaondoa madarakani iwapo watakosoa siasa za Washington. Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ni mmoja wa shakhsia hao. Abbas amekalia kiti cha Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuanzia mwezi Januari mwaka 2005 hadi sasa; na amekuwa akichukua hatua katika fremu ya maagizo yanayoainishwa na Washington. Pamoja na wananchi na makundi mengi ya Palestina kupinga pakubwa kufanyika mazungumzo baina ya serikali ya Palestina na utawala wa Kizayuni lakini Mahmoud Abbas na Serikali ya Ndani ya Palestina wameendeleza eti mazungumzo ya mapatano na utawala huo kwa kuungwa mkono pia na Marekani.  

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina 

Kupinga Mahmoud Abbas mpango wa kibaguzi uitwao "Muamala wa Karne" na hivi karibuni pia kupinga kwake mapatano ya kuanzishwa  uhusiano rasmi kati ya Imarati, Bahrain na utawala wa Kizayuni na vile vile kukatwa uhusiano wa Palestina na Washington na Tel Aviv kumeipelekea Washington kuanzisha mkakati wa kumuondoa madarakani Mahmoud Abbas na nafasi yake kumpatia Mohammed Dahlan. Mohammed Dahlan ni kati ya wanachama wa zamani wa harakati ya Fat-h; na ni miongoni mwa raia wa Palestina mwenye mchango muhimu katika kuanzishwa  uhusiano wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni. Baada ya harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) mwaka 2006 kulidhibiti eneo la Ukanda wa Ghaza na Mohammed Dahlan kukimbia eneo hilo; ushahidi na picha kutoka nyumbani kwake zimethibitisha namna  Dahlan alivyo na uhusiano mkubwa  na Wazayuni.  

Mohammed Dahlan, Kiongozi wa zamani wa harakati ya Fat-h kibaraka wa Marekani na Wazayuni 

Ni kwa kuzingatia hali hii ya mambo, ndio maana Marekani inafanya kila linalowezekana kumuondoa madarakani Mahmoud Abbas aliye na umri wa miaka 85 katika Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na badala yake kumweka uongozi Mohammed Dahlan ili kwa upande mmoja  kupunguza upinzani wa Wapalestina kwa mpango wa Muamala wa Karne na hivyo kufanikisha kuanzishwa uhusiano kati ya nchi za Kiarabu na Israel; na kwa  kwa mara nyingine tena kuibua migawanyiko na hitilafu kati ya makundi ya Kipalestina. Suala hilo la Muamala wa Karne na kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel sasa yamepelekea kuweko mshikamano wa kiasi fulani kati ya makundi ya Palestina kwa ajili ya kutetea maslahi na usalama wa Palestina. 

 

 

 

Tags

Maoni