Sep 20, 2020 11:21 UTC
  • Mirengo ya siasa Kuwait yakanusha kujiunga na mkumbo wa kutangaza uhusiano na Wazayuni

Mirengo mbalimbali ya kisiasa ya Kuwait imekanusha madai ya rais wa Marekani, Donald Trump aliyedai kuwa nchi hiyo nayo itajiunga karibuni hivi katika mkumbo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Juzi Ijumaa, Donald Trump alidai kuwa karibuni hivi Kuwait nayo itaingia katika mkumbo wa kutangaza uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni.

Leo shirika la habari la Quds Press limeinukuu mirengo 11 ya kisiasa ya Kuwai ikitoa tangazo la pamoja na sambamba na kulaani madai ya uongo ya Trump imeitaka serikali ya nchi hiyo nayo itangaze msimamo wake rasmi wa kupinga madai hayo ya Trump.

Mirengo hiyo ya kisiasa ya Kuwait pia imesisitiza kuwa, bunge la nchi hiyo nalo linapaswa kupitisha haraka sheria ya kupiga marufuku kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kama ambavyo imezitaka pia taasisi na makundi yote ya Kuwait kuchukua hatua za kimsingi za kuhakikisha sheria ya kupiga marufuku uhusiano na utawala wa Kizayuni inapasishwa na kuheshimiwa.

Trump na Netanyahu wakipigwa viatu

 

Jumanne iliyopita, mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walijipeleka kwa Donald Trump huko Marekani na kutia saini hati za kutangaza kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni tofauti kabisa na malengo ya wananchi wa Palestina.

Hadi hivi sasa ulimwengu mzima wa Kiislamu bali hata baadhi ya nchi zisizo za Waislamu, kama Afrika Kusini zinalaani kitendo hicho cha kisaliti cha Bahrain na Imarati.

Hatakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeitaja hatua hiyo kuwa ni hatari kubwa na ni zawadi ya bure ambayo Imarati na Bahrain zimeupa utawala wa Kizayuni.

Tags