Sep 21, 2020 02:26 UTC
  • Vurugu na machafuko Asia Magharibi; natija ya sera za Marekani

Marekani kwa mara nyingine tena imetoa taarifa ikiituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, eti inazusha vurugu na machafuko katika eneo la Asia Magharibi.

Taarifa ya taarifa hiyo iliyo dhidi ya Iran iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imedai kwamba, Iran inatumia utajiri iliyopata kupitia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa ajili ya kuzusha vurugu, mauaji na uharibifu kuanzia Yemen mpaka Iraq na Syria mpaka Lebanon.

Madai ya Marekani kwamba, Iran inazusha vurugu na machafuko katika eneo la Asia Magharibi ni urongo mtupu ambao ni ishara ya wazi ya kugonga mwamba sera za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; madai ambayo hata washirika wakongwe wa Washington barani Ulaya hawakubaliani nayo.

Hali ya mambo hii leo inayoshuhudiwa katika eneo la Asia Maghribi kabla ya yote imesababishwa na mikakati na stratejia tatu za Marekani ambazo ni vita, kuzusha mifarakano baina ya washindani na mataifa ya eneo na jambo la tatu ni kuligeuza eneo hili kuwa soko la silaha za Marekani; silaha ambazo hata Kongrsi ya nchi hiyo imekiri kinagaubaga kwamba, zimekuwa zikitumika dhidi ya raia.

 

Wananchi wa Yemen kama walivyo wananchi wa mataifa yote ya Kiarabu mwaka 2011 walishuhudia Mapinduzi ya Umma dhidi ya udikteta ambapo nao walianzisha harakati dhidi ya utawala wa dikteta Ali Abdallah Saleh. Takwa kuu la wananchi wa Yemen lilikuwa ni demokrasia katika nchi hiyo, jambo ambalo ndilo linalopigiwa upatu siku zote na Marekani.

Pamoja na hayo Marekani na waitifaki wake wa Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi walifanya kila wawezalo kuzuia juhudi za kupatikana demokrasia nchini Yemen. Hatimaye kuliitishwa uchaguzi wa kimaonyesho nchini Yemen ukiwa na mgombea mmoja wa urais na hivyo Marekani na waitifaki wake wakafanikiwa kumuweka madarakani Abdurabbuh Mansour Hadi.

Kile kilichopelekea kuibuka tena malalamiko nchini Yemen mwaka 2014 ni kushindwa Mansour Hadi kutekeleza matakwa ya wananchi na kuwa kwake tegemezi kikamilifu kwa madola ajinabi. Hatimaye Mansour Hadi alilazimika kujiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia, na hatamu za uongozi wa Yemeen zikashikwa na makundi mapya ikiwemo Harakati ya Wananchi ya Ansarullah.

 

Saudi Arabia ni muitifaki muhimu zaidi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Saudia ikipata himaya na uungaji mkono wa Marekani ikaanzisha vita dhidi ya Yemen. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali ya Donald Trump imetoa himaya na uungaji mkono wa kila upande kwa Saudia.

Natija ya vita hivyo ni kutokea maafa makubwa zaidi ya kibindamu ulimwenguni katika miongo ya hivi karibuni. Sababu kuu ya hali hii mbaya na ya kusikitisha ya Yemen, ni kupinga Marekani na Saudi Arabia ushikaji htamu tarajiwa wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, ambayo ina utambulisho wa kisiasa na kidini unaopingana kikamilifu na maslahi pamoja na malengo ya Washington na Riyadh

Hapana shaka kuwa, hata hali ya sasa ya Iraq ni natija ya vita na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu. Mwaka 2003 Marekani iliishambulia kijeshi Iraq kwa kisingizio cha kuweko nchini humo silaha za maangamizi ya umati. Lakini baada ya mwaka huo na kuendelea, kivitendo Iraq ikawa chini ya udhibiti na ukaliwaji mabavu wa Marekani. Kuundwa serikali isiyo thabiti nchini Iraq, kunaelezwa pia na weledi wa mambo kuwa ni matokeo ya uingiliaji mambo wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Majeshi ya Marekani nchini Syria

 

Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, Marekani haitaki kuona Iraq inakuwa na siasa na sera huru za kigeni, bali inataka nchi hiyo ifuate kikamilifu siasa na maagizo ya Washington, yaani Iraq iwe kama kile tunachokishuhudia leo kwa Imarati, Bahrain na nchi kadhaa za Kiarabu kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Sisitizo la mirengo na makundi mbalimbali ya Iraq juu ya kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo na kupinga kabisa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya nchi yao, kumekuwa sababu ya kuandaliwa njama na mipango haribifu na kutekekezwa hayo na mamluki na vibaraka wa Marekani nchini Iraq sambamba na kuzushwa vurugu na machafuko katika nchi hiyo.

Lebanon nayo kwa upande wake, nchi hii haikabiliwi na vita vya ndani bali inachoshumbuliwa nacho ni ushindani wa mirengo ya kisiasa kwa ajili ya kuwania madaraka. Mwaka 2018 ushindani huo ulikwenda sambamba na kuibuka na ushindi mrengo wa muqawama katika uchaguzi wa Bunge. Hata hivyo Marekani na waungaji mkono wa ndani na nje ya Lebanon Oktoba mwaka 2019 wakiwa na lengo la kufidia kushindwa kwao katika uchaguzi, walianzisha maandamano na mashinikizo dhidi ya muungano wa muqawama.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hali ya mambo inayoshuhudiwa hii leo nchini Lebanon ni natija ya uadui usio na mipaka wa Marekani na washirika wake dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq

 

Syria nayo mwaka 2011 ilishuhudia malalamiko ya wananchi, lakini baadaye malalamiko hayo yaligeuka na kuwa vita vya kigaidi dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad. Makundi ya kigaidi yakipata himaya na uungaji mkono wa mhimili wa Kimagharibi kwa uongozi wa Marekani, mhimili wa Kiarabu kinara wake akiwa Saudi Arabia na mhimili wa Kizayuni, yalifanya njama za kudhibiti maeneo ya Syria na kuandaa mazingira ya kuanzisha vita na umwagaji damu mkubwa lengo hasa likiwa ni kuindoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo.

Hata hivyo, uungaji mkono wa mhimili wa muqwama kwa uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vilevile himaya ya Russia, ulizuia vita vya kigaidi nchini Syria kufikia malengo yake ya kuiangusha serikali ya Rais Assad na kuigawa ardhi ya Syria.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kile ambacho kinafanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na waitifaki wake katika eneo hususan katika nchi nne za Yemen, Iraq, Lebanon na Syria, ni kujihami mkabala na hujuma za kukakariwa na mtawalia za Marekani na washirika wake dhidi ya mataifa hayo. Endapo hujuma na ushari wa Marekani na waitifaki wake wa kupenda vita utafikia tamati na kukaheshimiwa suala la haki ya wananchi ya kujiainisha hatima yao katika eneo hili hususan katika nchi hizo nne, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo itaunga mkono hilo kwa nguvu zake zote.

Tags

Maoni