Sep 21, 2020 03:16 UTC
  • Bin Zayed aishauri Pentagon ikihamishie Imarati kituo cha kijeshi cha Incirlik kilichoko Uturuki

Baadhi ya duru zimeripoti kuwa mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi Mohammad bin Zayed amefanya mashauriano na Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon juu ya mpango wa kukihamishia Imarati kituo cha anga cha jeshi la Marekani cha Incirlik kilichoko nchini Uturuki.

Tovuti ya habari ya Al Khaleej al Jadid imezinukuu duru hizo zikiripoti kuwa lengo la Bin Zayed la kufanya mashauriano hayo, pamoja na Imarati kusaini mkataba wa mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kutaka kuimarishwa uhusiano wa nchi yake na Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Imarati inapigania na kufuatilia pia kutekeleza miradi ya kiuchumi na kijeshi kwa kushirikiana na Pentagon na taasisi kubwa za kiuchumi na fedha za Marekani katika pwani ya kusini mwa Yemen na katika visiwa kadhaa vya nchi hiyo kikiwemo cha Socotra.

Mohammed bin Zayed

Seneta Ron Johnson, mjumbe wa kamati ya mahusiano ya nje ya Baraza la Seneti la Marekani aliwahi hapo kabla kusema kwamba, serikali ya Washington inachunguza mpango wa kuwahamisha askari wake walioko katika kituo cha kijeshi cha Incirlik kwa sababu ya sera zinazotia wasiwasi za Uturuki katika eneo la mashariki ya Bahari ya Mediterania.

Baada ya kutangaza uamuzi wa kiuhaini na usaliti wa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni, siku ya Jumanne iliyopita, Imarati na Bahrain zilisaini rasmi mikataba ya kuanzisha uhusiano huo wa kidiplomasia na kuutambua rasmi utawala bandia wa Israel, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington na kuhudhuriwa na rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa utawala huo haramu wa Kizayuni Benjamin Netanyahu.../ 

Tags