Sep 22, 2020 02:45 UTC
  • Umoja wa Mataifa na siku 2000 za vita vya Yemen

Vita vya kivamizi vilivyoanzishwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi maskini ya Kiislamu ya Yemen vimeshapindukia siku 2000. Matunda ya vita hivyo vya kidhalimu ni maafa makubwa ya kibinadamu katika nchi hiyo ya Kiarabu. Amma swali muhimu linalojitokeza hapa ni kwamba, Umoja wa Mataifa umefanya nini kuhusu vita hivyo katika kipindi hiki cha zaidi ya siku 2000 za tangu kuanzishwa kwake?

Umoja wa Mataifa ni chombo muhimu zaidi kimataifa. Jukumu kuu la umoja huo kwa mujibu wa hati ya kuasisiwa kwake, ni kulinda na kusimamia amani na usalama duniani. Vita vilivyoanzisha na muungano wa Saudia dhidi ya nchi maskini ya Yemen hapo tarehe 26 Machi, 2015 ambapo hadi sasa jinai za wavamizi hao zinaendelea baada ya zaidi ya siku 2000, ni ushahidi wa wazi kuwa Umoja wa Mataifa umeshindwa kutekeleza majukumu ya kuasisiwa kwake. Tangu vilipoanzishwa vita vya Yemen hadi hivi sasa, Umoja wa Mataifa umeshateua wajumbe watatu maalumu kufuatilia vita hivyo lakini hakuna lolote la maana uliloweza kufanya.

Jamal Benomar, mwanasiasa maarufu, alikuwa mjumbe wa kwanza kuteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa mjumbe maalumu wa vita vya Yemen, lakini hakudumu hata zaidi ya mwezi mmoja ila inaonekana mambo yalimshinda, hivyo alijiuzulu haraka na nafasi yake kuchukuliwa na Ismail Ould Cheikh Ahmed, mwanadiplomasia maarufu raia wa Mauritania.

Wavamizi wa Yemen wakiongozwa na Saudia wanafanya jinai kubwa dhidi ya watoto wadogo. Lakini Umoja wa mataifa umeshindwa kufanya chochote

Ould Cheikh Ahmed naye alifanya kazi hiyo kwa takriban miaka mitatu na baadaye kumkabidhi jukumu hilo Martin Griffiths, raia wa Uingereza. Pamoja na hayo, wajumbe wote hao wa Umoja wa Mataifa si tu wameshindwa kukomesha vita vya Yemen, bali hata hawajaweza angalau kupunguza tu makali ya vita hivyo. Wachambuzi wa mambo wanataja mambo kadhaa yanayosababisha jambo hilo.

Sababu ya Kwanza Muhimu ni kwamba kimsingi Umoja wa Mataifa umeshindwa kuwa mpatanishi mwadilifu katika vita vya Yemen. Mpatanishi mwadilifu asiyependelea upande wowote, kabla ya jambo lolote lazima afanye juhudi za kukomesha vita hivyo. Lakini Umoja wa Mataifa muda wote unataka kubadilisha mfumo wa kisiasa nchini Yemen kabla ya kumaliza vita kwanza. Tena mfumo unaopiganiwa na Umoja wa Mataifa ni ule ulioainishwa na Marekani na Saudi Arabia bila ya kujali matakwa hasa ya wananchi wa Yemen.

Mauaji ya umati msikitini Yemen yaliyofanywa na ndege za Saudi Arabia na wavamizi wenzake

Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ibrahim al Dailami, Balozi wa Yemeni nchini Iran amemshutumu na kumlaumu Martin Griffiths, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen kwa kuwapendelea wavamizi wa nchi hiyo. Amesema, Griffiths hajawahi kuwa mpatanishi mwadilifu hata mara moja. Misimamo yake ni sawa na ya Waingereza na hiyo ndiyo sababu ya kurefuka muda wa vita nchini Yemen. 

Kwa maneno ya wazi zaidi ni kwamba Umoja wa Mataifa ni sehemu ya wapinzani wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen. Ni kwa sababu hiyo ndio maana serikali hiyo ya San'aa haiuamini hata kidogo umoja huo.

Shule iliyosambaratishwa vibaya katika mashambulio ya Saudia nchini Yemen

Sababu ya Pili Muhimu ni kwamba Umoja wa Mataifa si chombo huru, bali kinaonesha wazi kuwa kinaburuzwa na baadhi ya nchi hasa madola makubwa ya kibeberu. Umoja huo ni tegemezi mno katika mambo yake yote hasa ya kisiasa na kifedha. Jambo pekee muhimu lililofanywa na Umoja wa Mataifa katika kipindi cha siku hizi zaidi ya elfu mbili za vita vya Yemen ni pale ulipojitutumua na kuliingiza jina la Saudi Arabia katika orodha ya wavunjaji wa haki za watoto wadogo. Pamoja na hayo, hata katika jambo hilo pia umoja huo umeshindwa kubakia katika msimamo wake kwani hatimaye umelazimika kuitoa Saudi Arabia kwenye orodha hiyo kutokana na mashinikizo ya kifedha na kisiasa ya Marekani na nchi za kibepari za Magharibi. 

Kwa kweli Umoja wa Mataifa umepewa jina tu la chombo cha kupigania haki, usalama na amani lakini uhakika wa mambo ni kwamba, kazi yake hasa ni kulinda manufaa ya kisiasa ya madola makubwa ya Magharibi na vibaraka wao na jambo hilo limeonekana kwa uwazi zaidi katika vita vya Yemen.

 

Maoni