Sep 23, 2020 01:35 UTC
  • HAMAS yaipa Israel miezi 2 ihitimishe mzingiro wa Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeupa utawala wa Kizayuni wa Israel muhula wa miezi miwili wa kuhitimishwa mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Khalil al-Hayya, mwanachama wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amesema utawala huo pandikizi umezuia kuingia katika eneo la Gaza misaada ya kibinadamu katika miezi kadhaa iliyopita, licha ya janga la corona.

Ameonya kuwa, iwapo utawala haramu wa Israel hautaki kuuhitimisha mzingiro wa Gaza kwa khiari, harakati ya HAMAS ina uwezo na nguvu kuulazimisha ufanye hivyo.

Mwezi uliopita, Fawzi Barhoum, msemaji wa HAMAS alisema kuwa, harakati hiyo ya muqawama itatumia suhula na nyenzo zote ili kuusambaratisha mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Israel inafanya jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina wa Gaza

Utawala wa Kizayuni wa Israel unalizingira eneo la Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006 wakati Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ilipoibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge la Palestina. Tangu wakati huo Israel imekuwa ikizuia kuingizwa bidhaa zote muhimu katika eneo hilo kama vile chakula, dawa, vifaa vya ujenzi na kadhalika. 

Umoja wa Mataifa mara kadhaa umesema katika ripoti zake kwamba, eneo la Ukanda wa Gaza linakabiliwa na maafa ya kibinadamu na kwamba, si mahala salama pa kuishi. 

Tags

Maoni